Habari

Refarenda ndiyo cheti rasmi cha 'talaka' ya UhuRuto?

August 29th, 2020 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

HUENDA refarenda iwe ndiyo barabara kuu ya kupisha utengano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Dkt William Ruto.

Uhusiano wao ambao kwa muda sasa umeonekana kujawa na baridi hasa katika awamu ya pili mamlakani unatazamiwa kuhitaji tu msukumo mdogo tu na usambaratike.

“Mimi binafsi nimekuwa nikisema kuna mambo ambayo hayaendi vizuri lakini sio yale ambayo hayawezi yakasuluhishwa. Kwa muda Wakenya wameshuhudia ushirika mpya ndani ya Jubilee na mambo yakifanyika tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali, hayo yote ni sawa hata kama ni kutukanwa na wadogo wangu ndani ya serikali,”akasema Dkt Ruto Alhamisi jioni katika mahojiano na runinga moja hapa nchini.

Lakini cha kuvutia wadadisi wa kisiasa ni wakati Dkt Ruto alisema kuwa “kwa sasa hatuoni haja kuu ya mabadiliko ya Katiba ikiwa ni harakati zitakazotii maslahi tu ya wachache”.

“Hatuwezi tukakubali kuingia katika sarakasi za kuundia watu watano nafasi kuwakilisha jamii tano ndani ya serikali huku jamii hizo zingine zote zikibaguliwa,” akasema Dkt Ruto.

Msimamo huu una uzito zaidi ikizingatiwa kuwa Jumatano Rais Kenyatta alitangaza kuwa kuna haja kubwa ya kupanua serikali “pale juu” ndipo Wakenya wengi zaidi wajihisi kuwa wanamiliki serikali na ni wadau katika utawala na uchumi wa nchi wala sio watakaoshindwa kwa kura kujihisi kuwa wageni katika taifa lao.

Dkt Ruto alisema ikiwa ni Wakenya wanasema hivyo “tuko sawa lakini ikiwa ni viongozi wachache wanaosukuma hilo sisi tutabakia pale sauti ya Mkenya itakuwa.”

Hali hii ya kuviziana kati ya Rais na naibu wake inaangazia mchezo wa paka na panya ambao unaelekeza ndoa yao kuibuka na talaka hadharani na hali ya mshikemshike kisiasa iibuke kati ya wafuasi wao na hatimaye taifa liingie katika siasa propa za 2022.

Cha kuvutia mno ni sadfa ya Dkt Ruto kujitokeza katika mahojiano hayo na kukariri tu msimamo uliotolewa na wanaompigia debe Mlima Kenya ambao Jumatano usiku walikuwa katika mkahawa mmoja mjini Sagana, Kaunti ya Kirinyaga; hali inayoangazia kuwa Dkt Ruto anapanga timu yake na anajadiliana nayo mara kwa mara.

Mkutano huo uliwaleta pamoja wabunge Ndindi Nyoro, Rigathi Gachagua na Alice Wahome wakiwakilisha Kiharu, Mathira na Kandara mtawalia, John Kiarie wa Dagoretti Kusini, Kimani Ichung’wa wa Kikuyu, Francis Theuri na Moses Gakuya wa Embakasi ya Kati na Mashariki mtawalia na Wangui Ngirici wa Kirinyaga miongoni mwa wengine waliokaribisha mwandani wa Dkt Ruto Rift Valley—Oscar Sudi – mbunge wa Kapseret.

Nyoro alifahamisha Taifa Leo kuwa walikuwa wanajipiga msasa kule wametoka, walikofika na wanakoelekea kama wandani wa serikali ya Jubilee na mirengo ibuka ndani ya serikali hiyo.

“Tulijadiliana kuhusu msimamo wetu wa kumuunga mkono Dkt Ruto kwa kila hali ya siasa zinazoendelea kuchezwa dhidi yake, nafasi yetu ndani ya serikali na chama cha Jubilee na siasa za kutulenga zinazoendelea kuchezwa, vita dhidi ya ufisadi na pia mvutano ulioko kati ya maseneta kuhusu mfumo wa ugavi pesa kwa ugatuzi.”

Walisema kuwa wataendelea kushirikiana na serikali ya Jubilee na kumuunga mkono Rais Kenyatta kuafikia malengo yake ya kiutawala “lakini kwa msingi kuwa yanayoendelezwa yanawiana na masharti ya kikatiba.”

Aidha, walisema kuwa watabakia katika kila kona ya siasa ndani ya himaya ya wananchi wala sio kwa matakwa ya wachache wanaotafutiwa au wanaojitafutia makuu; huu ukiwa ni mshale wa kisiasa ukielekezewa kinara wa ODM Raila Odinga na wengine kama Gideon Moi wa Kanu, Kalonzo Musyoka wa Wiper na Isaac Ruto wa Chama cha Mashinani ambao wako ndani ya Jubilee sasa kama washirika wa kiutawala na wanaochambuliwa kuwa wanajengwa kama mrengo wa kugombea urais 2022 dhidi ya Dkt Ruto.

Kuhusu refarenda, walisema watasubiri kuona kielelezo kitakachotolewa na wakishachambua waone ni matakwa ya wananchi yanayopendekezwa, na wananchi wenyewe waseme ni maoni yao, basi Dkt Ruto na wafuasi wake sugu watatii.

“Ikigundulika Wakenya hawatakuwa wamewakilishwa katika mapendekezo hayo na iwe ni mradi wa kundi la wachache kutuhadaa eti ni refarenda ya kitaifa ambayo itafadhiliwa na rasilimali za umma, basi ule upinzani tutazua haujawahi kushuhudiwa hapa nchini,” akasema.

Kuhusu hali kwamba Rais huenda apenyeze ajenda yake ya kung’oa mizizi ya Dkt Ruto kutoka serikali yake katika mabadiliko ya baraza la mawaziri yanayonukia, Nyoro alisema “sisi tushazoea.”

“Tumetengwa ndani ya Jubilee, tukatimuliwa kutoka nyadhifa bungeni; yaani madharau siku hizi ndiyo mengi kutoka kwa wanaojifanya ndio wawakilishi wa Rais katika chama na serikali. Sasa hicho kingine kinachoweza letwa kitushtue ni kitu gani?” akahoji Nyoro.

Walisema kuwa chama cha Jubilee kimetekwa nyara na matapeli, wakisistiza kuwa njia ya kugawa rasilmali kwa ugatuzi iwe ni ya kuunganisha Wakenya na kuwapa haki ya ushuru wao bila ubaguzi.

Nyoro alisema kuwa kubakia ndani ya Jubilee ndilo lengo kuu lakini “ikishindikana, kuna mianya tele ya kusaka utulivu na nafasi ya kukimbizana na ndoto zetu za kisiasa.”

Walisema kuwa kwa sasa “hali yetu ni ile ile tu ya kuyapa masuala yanayoendelea kuibuka ndani ya serikali macho tu, msimamo wetu ukiwa ni kuunga mkono yale mema lakini mabaya tumenyane nayo kwa wakati ufaao.”