Habari Mseto

Refarenda: Ruto kujipima nguvu katika ngome yake

November 26th, 2020 2 min read

ERIC MATARA na TOM MATOKE

UZINDUZI wa ukusanyaji sahihi za kufanikisha marekebisho ya katiba sasa umefungua wazi uwanja kwa Naibu Rais William Ruto kudhihirisha ubabe wake wa kisiasa katika eneo la Rift Valley.

Eneo hilo ni miongoni mwa yale yanayotarajiwa kuwa na upinzani dhidi ya refarenda, kwa vile Dkt Ruto anaaminika kuwa na ufuasi mkubwa.

Wandani wa Dkt Ruto katika ngome hiyo yake ya kisiasa tayari wameanza upya kuwakabili viongozi wanaounga mkono mchakato wa Mpango wa Maridhiano (BBI).

Katika ukanda huo, Kiongozi wa Kanu, Bw Gideon Moi, mwenzake wa Chama Cha Mashinani, Bw Isaac Ruto na Gavan wa Elgeyo Marakwet, Bw Alex Tolgos, wana jukumu la kushawishi wapigakura kutia sahihi kwenye mswada wa mapendekezo ya kurekebisha katiba.

Mswada huo ulizinduliwa rasmi Jumatano na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, katika hafla ambayo Dkt Ruto hakuhudhuria.

Tayari, Gavana wa Nandi, Bw Stephen Sang, aliye mwandani wa Naibu Rais ameonya kwamba hataruhusu ukusanyaji wa saini za kuunga BBI katika kaunti yake.

“Katika Kaunti ya Nandi hatutakubali. Mtu asijaribu kuja kutafuta saini hapa, hakuna mtu atapeana saini katika kaunti yetu ya Nandi, kwenda tafuta mahali kwingine,” alisema Bw Sang.

Matamshi hayo tayari yamesababisha Tume ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kusema itamuita Bw Sang kumhoji kufuatia kauli hiyo.

“Kaunti ya Nandi ni miongoni mwa maeneo saba ambayo NCIC imetambua kama yanayoweza kukumbwa na fujo kuhusu BBI na kwenye uchaguzi mkuu ujao. Tutamuita Gavana Sang kuandikisha taarifa,” alisema Kamishna wa NCIC, Bw Abdulaziz Farah.

Tolgos asema mswada una manufaa

Wakati huo huo, Bw Tolgos pia alipuuzilia mbali wafuasi wa ‘Tangatanga’ wanaopinga kura ya maamuzi na kuwataja kuwa wabinafsi kwani mswada uliopendekezwa una manufaa chungu nzima hasa kwa serikali za kaunti.

“Tunawaomba wasitutatize tunapohamasisha umma, nasi pia tutawapa muda kueleza misimamo yao wakitaka hivyo,” akasema.

Bw Sang alisisitiza kuna changamoto tele zinazohitaji kutatuliwa na viongozi wakati huu wala si kujihusisha kwa kura ya maamuzi.

Magavana wengine wanaounga BBI eneo la Rift Valley ni Lee Kinyanjui (Nakuru), Samuel Tunai(Narok), Joseph ole Lenku(Kajiado), Patrick Khaemba (Trans Nzoia), Ndiritu Muriithi (Laikipia) na Prof John Lonyangapuo (Pokot Magharibi).

Kwa kuwa eneo la Rift Valley ni ngome yake ya kisiasa, Dkt Ruto huenda akaamua kudhihirisha ubabe wake kwa kuzima shughuli hiyo eneo hilo.

Mnamo Jumatano, Naibu Rais aliendelea kuelezea matumaini kwamba hata baada ya kuzinduliwa kwa ukusanyaji sahihi bado kuna nafasi ya kupatikana kwa muafaka ili kusiwe na kura ya maamuzi ya kuleta migawanyiko nchini.

“Hata baada ya kuzinduliwa kwa ukusanyaji sahihi, naamini bado kuna nafasi ya kupatikana kwa maelewano ili kufanyike refarenda itakayowapa Wakenya nafasi ya kujieleza bila ushindani. Umoja na nguvu ndio inahitajika katika vita dhidi ya Covid-19 na ukarabati wa uchumi,” akasema Dkt Ruto kupitia akaunti yake ya Twitter.

Hii ni ishara kwamba hakuridhishwa na mabadiliko ambayo yalifanywa katika ripoti ya BBI na mswada wa marekebisho wa Katiba, na ikizingatiwa kwamba meli ya refarenda tayari imeng’oa nanga, huenda asiwe na budi ila kuendeleza kampeni za kupinga marekebisho ya katiba.