Michezo

Refarii adai mashabiki wengi wa Man City ni wanafunzi, wa Liverpool ni wakongwe

May 10th, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MASHABIKI wengi wa Manchester City nchini Kenya ni wanafunzi katika shule za msingi, sekondari na taasisi za kitaaluma, amesema refarii wa kiwango cha Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL) Bw Jimmy Kamande.

Bw Kamande ambaye ni mwalimu kitaaluma, anasema kwamba mashabiki hao ni wale waliopata Man City ikipapura wapinzani bila huruma na kutwaa mataji, na ndipo wakaingia kuishabikia wakijihusisha na ufanisi.

Bw Kamande ambaye umaarufu wake wa kipenga umempa jina la majazi la yule refarii Mwitaliano Pierluigi Collina, alisema watoto hao mashabiki wamejiunga na timu hiyo ya Man City katika kipindi cha misimu mitano iliyopita.

Refarii Jimmy Kamande. PICHA | MWANGI MUIRURI

Alidai mashabiki wengi wa Liverpool ni wakongwe.

“Wafuasi wa Liverpool wengi ni wakongwe, wale wa Manchester United ni wazee ambao sanasana huwa ni wazee kuwaliko wale wa klabu ya Arsenal,” akasema Bw Kamande.

“Lakini mashabiki wa Man City ni wadogo sana kiumri wakifuatiwa na wa Chelsea ambao ni wa pili kwa udogo kiumri,” akafafanua.

Naye Askofu Yohana Gichuhi, ambaye ni shabiki sugu wa Arsenal, anasema kwamba mashabiki wa Man City nchini Kenya ni vigumu kujadiliana masuala ya mpira kwa kuwa hawana historia za kumbukumbu za ligi yoyote duniani.

“Hao ni wale hata leo hii wakisikia Burnley au Sunderland imechukua ligi, watakimbia kusema wao ni mashabiki sugu wa klabu hizo. Ni wale ambao haja yao ni kuhusishwa na umaarufu,” anasema Bw Gichuhi.

Kwa sasa, Man City ndio klabu yenye nafasi bora zaidi ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya sita mfululizo.

Arsenal na Liverpool licha ya kuwa na nafasi pia, zinategemea Man City ichapwe katika mojawapo ya mechi zake tatu zilizosalia.

Mwanafunzi Stephen Kogi anayesomea taaluma ya Biashara katika Chuo Kikuu cha Murang’a, kando na kuwa shabiki wa Man City anasema kwamba “hii ni timu ya kisasa na wala sio ya mashabiki kienyeji kama wa Arsenal, Liverpool na Man U”.

Mwanafunzi huyo anasema kwamba “Chelsea ndio inatufuata kwa kuwa na bongo za kisasa”.

Anadai tofauti hizi za kiumri hutambulisha mashabiki wa Liverpool nchini kama wanaopenda kutoa ushauri, wa Manchester United kama wanaojiona wababe huku wa Arsenal wakihusishwa na “kujua sana”.

Bi Stephanie Naixx ambaye pia ni mwanafunzi katika chuo hicho, anasema kwamba “sisi vijana wa Man City tunapenda usasa na kupiga luku”.

“Sisi Man City ni mali safi na timu nyingine zisubiri na kushuhudia tukinyanyua taji kila msimu,” anasema Stephanie.