Refarii Omagwa ajiwekea malengo ya kufika mbali katika soka

Refarii Omagwa ajiwekea malengo ya kufika mbali katika soka

Na LAWRENCE ONGARO

MAREFARII huwa wanaendesha shughuli nzito viwanjani ambapo uvumilivu mkubwa unahitajika.

Hayo yamenenwa na refarii stadi Christopher Omagwa, 32, kutoka kaunti ndogo ya Ruiru.

Refa huyo anasema ari kuu iliyomchochea kujiunga na kozi ya urefa ni kutokana na upungufu wa marefarii katika eneo hilo la Ruiru na vitongoji vyake.

“Mimi hapo awali nilikuwa shabiki sugu wa soka na nilizoea kuhudhuria mechi za Ligi Kanda ya Aberdare Kati mwaka wa 2015 hadi 2016,” alisema refa Omagwa.

Hata hivyo anasema wakati huo kuna refa stadi aliyejulikana kama Issac Kiriara, aliyenifurahisha kwa maamuzi yake na ndipo akavutiwa kuwa refa.

Refarii stadi Christopher Omagwa (kati). Picha/ Lawrence Ongaro

Anazidi kueleza kuwa ilipofika mwaka wa 2017 Omagwa aliamua kuingia darasani kujifunza kazi ya urefa.

Anampongeza mwenyekiti mkuu wa marefarii tawi la Aberdare hapo awali, marehemu Ruel Ndirangu, ambaye kwa muda wa miezi sita mfululizo alimpatia mafunzo tosha hadi akafika kiwango cha kuamua mechi za Ligi ya Kitaifa Daraja la Pili.

“Kama sio ujuzi wa hali ya juu wa marehemu Ndirangu, singefika mahali nilipo kwa sasa. Kwa hivyo. najivunia jambo hilo,” anafafanua Omagwa.

Pia anamsifu katibu wa kanda ya Kati Paul Gathirua, ambaye ni mratibu wa mechi zote zinazochezwa eneo hilo.

Anamtaja kama afisa anayeelewa majukumu yake kwani kila timu hupokea ratiba ya mechi zao kila wiki bila kuchelewa.

“Endapo afisa yeyote atapata matatizo kuhusu michezo ya soka, yeye huwa mstari wa mbele kutatua shida hizo,” anaeleza refa huyo.

Analitaja mwenyekiti wa marefarii kaunti ndogo ya Ruiru Simon Kariuki kama afisa mwenye maono.

Anasema kwa chini ya miaka mitatu afisa huyo ameweza kuwanoa marefarii wapatao 34 ambapo wanawake ni saba (7) katika kaunti ndogo ya Ruiru.

Anatoa wito kwa makocha wote popote walipo kudumisha nidhamu miongoni mwa klabu zao.

“Wakati mwingi sisi kama marefa tunapitia changamoto tele ya utovu wa nidhamu miongoni mwa wachezaji. Unapotoa uamuzi wachezaji wengine hupinga uamuzi huo, jambo linalotia wasiwasi,” akafafanua refa huyo.

Anatoa wito pia kwa marefarii wenzake wawe wakipitia masomo ya kila mara ili kuelewa sheria mpya za soka zinavyotolewa kila mara.

“Tungetaka makocha popote walipo wawe na ushirikiano mwema na marefarii ili kuinua hali ya soka nchini. Hakuna haja ya mivutano ya kila mara viwanjani kunapotokea maamuzi muhimu ya soka,” akasema refa huyo.

Mwamuzi huyo ambaye amejitolea mhanga anasema azma yake kuu ni kupanda ngazi pole pole hadi kuwa mwamuzi wa kimataifa wakati wake ukifika.

  • Tags

You can share this post!

Messi afunga mabao mawili na kusaidia PSG kutoka nyuma na...

Akamatwa na bastola feki na kutupwa jela

T L