Habari MsetoSiasa

REFERENDA: Maina Njenga aapa kupigia debe marekebisho

October 23rd, 2018 2 min read

STEVE NJUGUNA na GEORGE SAYAGIE

KIONGOZI wa zamani wa kundi la Mungiki Maina Njenga ameapa kutumia vuguvugu lake la Amani Sasa Foundation, kuhimiza Wakenya kuunga mkono kubadilishwa kwa Katiba kupitia kura ya maamuzi.

Bw Njenga anataka Katiba ibadilishwe ili kubuni cheo cha waziri mkuu na manaibu wake wawili kabla ya uchaguzi wa 2022.

Akizungumza mjini Nyahururu, wikendi, Bw Njenga alisema katiba ya sasa ni mzigo kwa walipa ushuru kwani nchi inatumia kiasi kikubwa cha fedha kulipa mishahara wafanyakazi wa serikali ya kitaifa na kaunti.

“Katiba ya sasa ni mzigo kwa Wakenya, walipa ushuru wanaumia kiasi kikubwa kulipa wafanyakazi wa serikali licha ya gharama ya maisha kuongezeka kila uchao,” akasema Bw Njenga.

Alisema vuguvugu lake pia linapigania kuleta amani na usawa nchini.

“Tunapigania katiba ambayo itawezesha Wakenya kutangamana. Hatutaki kuona katiba ambayo itasababisha nchi kugawanyika kwa misingi ya kikabila baada ya uchaguzi,” akasema.

Kabla ya kundi la Mungiki kuharamishwa, Bw Njenga alikuwa na uungwaji mkubwa miongoni mwa vijana haswa kutoka eneo la Mlima Kenya, Nairobi na Nakuru. Alidai kuwa angali na ushawishi mkubwa miongoni mwa vijana.

Alisema anaunga mkono kupunguzwa kwa kaunti, maeneobunge na kufutiliwa mbali kwa baadhi ya nyadhifa.

Anataka kuwepo na rais, naibu wa rais, waziri mkuu na manaibu wake wawili wote kutoka katika jamii mbalimbali

“Tunahitaji kuongeza nyadhifa serikalini. Ninapendekeza kuwa baadhi ya kaunti ziunganishwe na ziwe 12 pekee. Tupunguze idadi ya maeneobunge hadi 150,” akasema mwasisi huyo wa vuguvugu la Amani.

Pendekezo hilo la Bw Njenga, limeungwa na baadhi ya viongozi.

Mjini Narok, wabunge wawili waliunga mkono wito wa kufanyika kwa kura ya maamuzi.

Wakizungumza katika maeneo tofauti, mbunge wa ODM Moitalel Ole Kenta (Narok Kaskazini) na mwenzake wa Jubilee Gideon Konchellah (Kilgoris) walisema kuwa kura ya maamuzi ni lazima ifanyike kabla ya 2022.

“Urais umekuwa ukichukuliwa na watu wa kutoka jamii mbili pekee tangu Kenya kupata uhuru. Hivyo tunaunga mkono kubuniwa kwa afisi ya waziri mkuu na manaibu wake wawili,” akasema Bw Kenta.