Habari MsetoSiasa

Referenda ni nafasi murua kwa wanawake kutetea jinsia – Karua

October 15th, 2018 2 min read

IRENE MUGO na OSCAR KAKAI

KIONGOZI wa chama cha Narc Kenya, Bi Martha Karua, amewataka wanawake kutetea usawa wa jinsia kwenye mageuzi ya Katiba yanayopendekezwa.

Alisema anaunga wito wa kura ya maamuzi ambapo maeneobunge yatabadilishwa kuwa wadi kila moja ikiwakilishwa na mwanamume na mwanamke kama njia moja ya kuhakikisha usawa wa jinsia.

“Mageuzi ya Katiba yanafaa na yanapaswa kutumiwa kujaza pengo la jinsia,” alisema. Alikuwa akihutubia madiwani wanawake wa bunge la Kaunti ya Nyeri walipozindua mwongozo wao.

Alipendekeza mageuzi ya Katiba ambapo wanawake watakuwa wakiwa wagombeawenza ikiwa anayegombea kiti cha urais ni mwanamume.

“Kama wanawake, ni lazima tuchangie katika mageuzi ya Katiba na kuhakikisha tumefaidika na pia tuhakikishe Katiba imebadilishwa ili mgombea urais akiwa mwanamume, mgombeamwenza awe ni mwanamke na iwapo ni mwanamke mgombea mwenza anafaa kuwa mwanamume,” alisema Bi Karua.

Alipendekeza kuwa wabunge na maseneta hawafai kuzidi 188 badala ya 416 ilivyo kwa sasa.

Alisema maeneobunge 290 yanapaswa kubadilishwa kuwa wadi kila moja na yawakilishwe na mwanamume na mwanamke ili kuwe na usawa wa jinsia.

Aidha, Bi Karua alisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inafaa kufanyiwa mageuzi kabla ya nchi kuandaa kura ya maamuzi.

“Huu ndio wakati wa kurekebisha mambo kwa kupunguza bajeti ya IEBC. Uchaguzi Kenya unagharimu pesa nyingi kuliko nchi zinazoendelea ulimwenguni,” alisema.

Kwingineko, walimu wa Pokot Magharibi wametishia kuunga mkono pendekezo la kurekebisha Katiba ili kuirejesha Tume ya Huduma kwa walimu nchini (TSC) chini ya wizara ya Elimu.

Waliapa kushiriki mgomo wa kitaifa kulemeza mitihani ya kidato cha nne na darasa la nane, ikiwa mkutano wao na mwajiri wao ambao umepangwa kufanyika Jumatano wiki hii hautazaa matunda.

Wakihutubia wanahabari mjini Kapenguria, walimu hao walitoa wito kwa TSC kuipiga msasa sera yake kuhusu uhamisho ili kuimarisha utendakazi wa walimu.

Katibu wa Knut tawi hilo, Bw Martin Sembelo, aliwaongoza walimu kuilaumu TSC kwa kupuuza mahangaiko wanayopitia.

“Ikiwa TSC haitaelewa kuwa walimu ndio walichangia tume hiyo kuwa huru kwenye Katiba ya mwaka wa 2010, tutairudisha kwenye wizara ambapo matakwa ya walimu yanaweza kusikilizwa. Sera hiyo inafaa kuangaliwa na kuchunguzwa kwa kina,” alisema.

Bw Sembelo alisema kuwa walimu wengi wameshindwa kufika katika vituo mbalimbali kutokana na suala la umri na wengi wamekuwa wagonjwa.

Mjadala kuhusu kuifanyia marekebisho Katiba umeshika kasi, na sasa walimu nao wanasema watatumia fursa hii kupendekeza TSC isiwe tume huru.

Wanaamini kuwa endapo itakuwa chini ya wizara ya Elimu, itakuwa ikibuni na kutekeleza sera chini ya uangalizi wa wizara, ambayo itakuwa ikitoa ushauri unaofaa kuhusu sera hizo.