HabariSiasa

REFERENDA: Raila amchenga Uhuru

October 15th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya kinara wa ODM, Raila Odinga kupigia debe marekebisho ya Katiba imekiuka makubaliano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta kwenye mwafaka wao wa maelewano.

Kulingana na mwafaka huo ulioafikiwa Machi 9, miongoni mwa waliyokubaliana ni kubuni kamati ya watu 14 ambayo ingekuwa na jukumu la kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya, ili waeleze wanayotaka yafanyike katika kujenga uwiano nchini.

Kamati hiyo ilibuniwa ikiongozwa na Wakili Paul Mwangi na Balozi Martin Kimani na ndiyo ingetoa mwelekeo wa iwapo Katiba itafanyiwa mageuzi, aina ya mageuzi wanayotaka Wakenya na lini.

Hata hivyo, hata kabla ya kamati hiyo kuanza kukusanya maoni ya wananchi, Bw Odinga alianza kupigia debe kura ya maamuzi. Hii inaonekana kama mbinu ya kuwekea kamati hiyo ajenda na kushawishi mapendekezo yake.

Kwa upande wake Rais Kenyatta amekuwa kimya kuhusu mjadala wa marekebisho ya Katiba.

Bw Mwangi, ambaye ni mwandani wa Bw Odinga na wakili wake, anasema ni mapema kuendeleza mjadala kuhusu kura ya maamuzi.

“Ninahisi kwamba Rais Kenyatta na Bw Odinga hawatasita kufanya mageuzi yanayofaa baada ya kamati kukusanya maoni,” alisema Bw Mwangi kwenye mahojiano na runinga ya Citizen.

Kulingana na Dkt Edward Kisiang’ani, mhadhiri na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, kwa kuzua mjadala wa Katiba hata kabla ya ripoti ya kamati, Bw Odinga anacheza sarakasi za siasa.

“Kwanza anaonekana kutoelewa anachotaka katika kura ya maamuzi. Tunaona mtu anayetaka kuweka vipengele katika Katiba kulinda maslahi yake ya kibinafsi na hii huenda isifurahishe Wakenya,” alisema Dkt Kisiang’ani.

Bw Odinga anaonekana kujikanganya katika msimamo wake kwani amekuwa akikiri kwamba ni kamati hiyo ya watu 14 itakayotoa ripoti ya mwisho kuhusu mageuzi ya kikatiba ambayo Wakenya watataka.

“Wakenya wakisema tupige nyundo hapa, tulainishe pale, hakuna makosa,” kiongozi huyo wa upinzani amenukuliwa akisema mara kwa mara.

Kwenye hafla zingine amekuwa akisisitiza kuwa ni sharti mageuzi ya Katiba yafanyike.

Rais Kenyatta kwa upande wake ameepuka suala hilo akisisitiza kuwa lililo muhimu kwake kwa wakati huu ni kuwahudumia Wakenya.

“Uhuru anafahamu kwamba wanasiasa wana misimamo yao na yuko makini sana kutomwaga mtama kuhusu msimamo wake kabla ya kamati kukusanya maoni kutoka kwa Wakenya,” alisema mbunge mmoja wa chama cha Jubilee.

Anasema Rais Kenyatta hataki suala hilo lionekane kama maafikiano ya watu wawili na ndio sababu waliunda kamati ya watu 14 kukusanya maoni ya Wakenya.

Msemaji wa Ikulu Kanze Dena pia alisema hawezi kueleza msimamo wa Rais kwa sababu hajazungumzia suala hilo.

Kulingana na mdadisi wa masuala ya kisiasa Mutahi Ngunyi, ikiwa Rais na na Bw Odinga wanaunga kura ya maamuzi hakuna atakayezuia ifanyike.

Hata hivyo, aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale anahisi kwamba mbio za Bw Odinga huenda zikamtumbukiza pabaya.

“Raila alikubali kutumiwa na serikali ya Jubilee. Wakati wake wa kuaibika utafika na atagundua hakuna chake,” alisema Bw Khalwale.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna naye anakiri kwamba kura ya maamuzi itategemea jopo la watu 14.