Habari MsetoSiasa

REFERENDA: Thirdway Alliance yakusanya sahihi 617,800

October 30th, 2018 1 min read

Na MILLICENT MWOLOLO

CHAMA cha Thirdway Alliance kimekusanya sahihi 617,800 za wapigakura wanaotaka marekebisho ya katiba kufikia sasa, Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw Fredrick Okango amesema.

Sahihi hizo zilikusanywa kutoka maeneo ya Naivasha Nakuru, Molo, Thika, Kiambu, Isiolo, Uasin Gishu, Eldoret, Iten, Turbo, Elgeyo Marakwet, Baringo na Samburu.

“Hizi ni sahihi zilizothibitishwa ambazo pia zimehifadhiwa kidijitali. Tuna sahihi nyingine zaidi ambazo hazijathibitishwa,” akasema.

Bw Okango aliongeza kuwa wiki hii chama hicho kitaelekea Kaunti za Kisumu, Siaya, Nyamira, Bomet na Narok katika juhudi zake za kutafuta sahihi za wapigakura milioni moja ndipo chama kipige hatua mbele katika harakati zake za kutaka katiba irekebishwe.

Chini ya wito wa “Punguza Mzigo”, chama hicho kilianza wito wa marekebisho mwaka uliopita kwa lengo kuu la kupunguza idadi ya viongozi wa kisiasa hasa kutaka wabunge wapunguzwe kutoka 416 hadi 194.

Vile vile, chama hicho kinachoongozwa na Dkt Ekuru Aukot kinataka kaunti 47 zilizopo zigeuzwe kuwa maeneobunge ambapo kila moja litakuwa na mbunge wa kiume na wa kike katika Bunge la Taifa, na vivyo hivyo katika Seneti.

Wabunge sita watateuliwa kuwakilisha makundi maalumu.

“Hivi sasa Kenya ina uwakilishi wa kisiasa uliopita kiasi. Kura ya maamuzi kubadilisha hili itasaidia kupunguza gharama ya kuendeleza shughuli za bunge kutoka Sh36.8 bilioni hadi Sh5 bilioni kila mwaka. Kwa hivyo mlipa ushuru atapunguziwa gharama ya Sh31.8 bilioni kila mwaka,” akasema Bw Okango.

Lengo lao pia ni kutaka kuwe na awamu moja ya urais inayodumu kwa miaka saba ili kukabiliana na ghasia zinazoshuhudiwa kila wakati wa uchaguzi wa urais.