Reggea ilizma Ajenda Nne Kuu za Rais – Ruto

Reggea ilizma Ajenda Nne Kuu za Rais – Ruto

Na SAMMY WAWERU

SALAMU za maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga zilichangia kusambaratika kwa mipango ya Ajenda Nne Kuu za Rais, Naibu wa Rais William Ruto amesema.

Dkt Ruto amesema utekelezaji wa ajenda hizo ungekuwa umepiga hatua nyingi, ila handisheki iliharibu maendeleo.

“Mipango ya Ajenda Nne Kuu ilisambaratishwa na hawa watu wa reggae. Kwa sasa imesimama,” Dkt Ruto akasema, akionekana kuelekeza lalama zake kwa upinzani.

Rais Kenyatta na Bw Odinga, walitangaza kuzika tofauti zao za kisiasa Machi 2018, ambapo wawili hao wamekuwa wakishirikiana kuendesha mikakati ya serikali.

Ni kupitia Handisheki, Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), ambayo inapendekeza mabadiliko ya Katiba ilibuniwa.

Hatma ya mswada huo maarufu hata hivyo ipo mikononi mwa mahakama ya rufaa, baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kukata rufaa uamuzi wa mahakama kuu iliyouharamisha kufuatia pingamizi ya baadhi ya wanaharakati na mashirika.

Kulingana na Dkt Ruto, salamu za maridhiano zimechangia kuathirika kwa utekelezaji wa sera za Jubilee.

“Kwa sasa tunatumia kima cha Sh15 bilioni kuwapa chakula cha msaada wanaosakamwa na njaa. Mikakati tuliyoweka awali, tungezitumia kuboresha kilimo,” akasema, akiongeza kuwa endapo ataingia Ikulu 2021 ataweka mipango maalum kuboresha sekta ya kilimo kukabili baa la njaa nchini.

Aidha, alisema mgao huo, badala yake atautumia kupiga jeki walioathirika kuendeleza kilimo.

“Sasa hawa watu wa reggae wanaongea kuhusu mfumo wa kubadilisha Katiba, mfumo ambao haujafanya kazi kwa zaidi ya miaka 50,” akasema.

You can share this post!

Serikali yakiri kudaiwa Sh16m za usalama wa baharini

Ujenzi wa daraja Starehe kucheleweshwa