Habari

Rekodi muhimu kuhusu Sharon na Melon zakosekana hospitalini

June 18th, 2019 1 min read

Na BENSON AMADALA

MAAFISA katika hospitali ya Kakamega Referral Jumatatu walisema kuwa rekodi muhimu kuhusu pacha waliozaliwa hospitalini humo lakini wakatenganishwa miaka 19 iliyopita hazipatikani.

Baada ya siku mbili za kuzitafuta, usimamizi wa hospitali hiyo ulipata baadhi ya rekodi ambazo zinadhihirisha kuwa Sharon Mathius na Melon Lutenyo walizaliwa humo.

Lakini waziri wa afya wa kaunti hiyo Rachael Okumu alisema rekodi zingine ambazo zingeonyesha kilichotendekeka baada ya pacha hao kuzaliwa huenda ziliharibiwa baada ya muda uliotengwa kisheria kukamilika, na hivyo ni vigumu kujua kilichotokea.

Bi Okumu alisema kuwa hospitali hiyo haina chochote cha kuficha kuwahusu pacha hao, na wakaamua kupokeza wapelelezi nyaraka zilizopatikana kwa uchunguzi zaidi.

Wakili wa kaunti hiyo, Moses Sande alisema rekodi za matibabu huwa si za siri na kuwa zinaweza kuharibiwa baada ya miaka saba.

“Wakati huo, hospitali hii ilikuwa ikisimamiwa na serikali kuu na kuna uwezekano mkubwa kuwa rekodi kuwahusu pacha hao ziliharibiwa,” akasema Bw Sande.

Inashukiwa kuwa hali ya utepetevu katika hospitali hiyo ndiyo iliyosababisha pacha hao kutenganishwa mara baada ya kuzaliwa.

Uchunguzi wa DNA uliofanyiwa Sharon na Melon na shirika la Lancet ulionyesha kuwa wasichana hao ni pacha kwa asilimia 99.9.

“Bi Rosemary Khaveleli Onyango ndiye mama wa pacha hao, ambao matokeo yanaonyesha uwezekano wa asilimia 99.9 kuwa ni pacha,” ripoti ya uchunguzi huo ikasema.

Ripoti hiyo ilisema kuwa Bi Khaveleli si mamake Mevis Imbayi, ambaye amekuwa akiishi naye kama bintiye kwa miaka hiyo 19.

Badala yake, uchunguzi huo ulionyesha kuwa mamake Mevis ni Bi Angeline Omina na babake ni Wilson Luttah Maruti.

Pacha hao walikutana Desemba 2018 katika kituo cha basi mjini Kakamega baada ya kusikia ripoti walipokuwa katika shule wanakosomea kuhusu kufanana kwao kutoka kwa wanafunzi na walimu.

Sasa inasubiriwa uamuzi ambao familia hizo mbili zitachukua baada ya kufahamu ukweli.