Michezo

REKODI? Ronaldo alenga kuvunja rekodi ya dunia ya ufungaji bora katika soka ya wanaume

November 19th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

NYOTA Cristiano Ronaldo ameahidi anatia zingatio katika kuvunja rekodi ya dunia ya ufungaji bora katika soka ya wanaume baada ya kupachika wavuni bao lake la 99 mnamo Jumapili na kuongoza Ureno kupepeta Luxembourg 2-0 katika kivumbi cha kufuzu kwa fainali za Euro 2020.

Ronaldo anasalia na mabao 10 pekee kufikia rekodi ya dunia ambayo kwa sasa inashikiliwa na nguli wa soka ya Iran, Ali Daei aliyefunga magoli 109 katika enzi yake ya usogora. Hadi kufikia sasa mwaka huu, Ronaldo ameifungia timu yake ya taifa jumla ya magoli 14.

“Rekodi zote huwekwa na binadamu. Binadamu wao hao ndio walio na uwezo wa kuzivunja. Nami nimepania kuvunja rekodi ya dunia ya ufungaji bora katika soka ya wanaume,” akatanguliza fowadi huyo wa Juventus na timu ya taifa ya Ureno.

Wakicheza dhidi ya Luxembourg mnamo Jumapili, Ureno waliwekwa uongozini kupitia kwa Bernardo Silva wa Manchester City kabla ya Ronaldo kuongeza la pili mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ureno ambao ni mabingwa watetezi wa Euro, walijibwaga katika mchuano huo dhidi ya Luxembourg wakiwa na ulazima wa kusajili ushindi ili kujikatika tiketi ya kunogesha fainali zijazo.

Nafasi ya pili

Chini ya kocha Fernando Santos, Ureno waliotawazwa mabingwa wa Euro mnamo 2016, walikamilisha kampeni zao za Kundi B katika nafasi ya pili kwa alama 17, tatu nyuma ya Ukraine walioongoza kundi hilo. Katika mchuano wao wa mwisho, Ukraine walilazimishiwa na Serbia sare ya 2-2. Luxembourg wanashikilia nafasi ya nne kwa alama nne, tatu zaidi kuliko Lithuania.

Ronaldo atalazimika sasa kusubiri hadi mwezi Machi 2019 kwa fursa ya kuwa mwanasoka wa pili katika historia kufunga jumla ya mabao 100 katika soka ya kimataifa.

Mnamo Alhamisi, Ronaldo alifunga hat-trick yake ya tisa na ya saba tangu ahitimu umri wa miaka 30 alipokuwa akiwajibikia timu ya taifa dhidi ya Lithuania.