Renato Sanches sasa andazi moto linalowaniwa Arsenal na Liverpoo

Renato Sanches sasa andazi moto linalowaniwa Arsenal na Liverpoo

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL wamejitosa katika vita vya kuwania huduma za kiungo mvamizi wa Lille na timu ya taifa ya Ureno, Renato Sanches anayehusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua kambini mwa Arsenal.

Kocha Mikel Arteta amekiri kwamba kubwa zaidi katika mipango yao muhula huu ni kujinasia maarifa ya Sanches na Manuel Locatelli ili kujaza nafasi za Matteo Guendouzi na Granit Xhaka. Huku Guendouzi akitarajiwa kuyoyomea Ufaransa kuvalia jezi za Olympique Marseille, Xhaka anahusishwa pakubwa na AS Roma ya Italia.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe nchini Ufaransa, Arsenal wako radhi kuvunja benki na kutoa ofa ya Sh8.9 bilioni kwa ajili ya Sanches ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Bayern Munich ya Ujerumani. Liverpool wameahidi kuboresha zaidi ofa hiyo kwa kuweka mezani Sh9.2 bilioni.

Lille wanatarajiwa kuagana pia na kiungo Xeka anayehusishwa pakubwa na Napoli ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A). Lille waliotawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo 2020-21, tayari wamekatiza uhusiano na mkurugenzi wa soka Luis Campos na kocha Christophe Galtier.

Sanches, 23, huwa mwepesi wa kupata majeraha mabaya kutokana na mtindo wa kucheza kwake. Sogora huyo ambaye ana mazoea ya kumiliki mpira kwa muda mrefu na kupiga chenga nyingi za maudhi, hajawahi kusakata zaidi ya mechi 24 katika kampeni za msimu mmoja.

Kuja kwake ugani Emirates kutapiga jeki safu ya kati ya Arsenal ambao kwa sasa wanategemea pakubwa maarifa ya Thomas Partey wa Ghana aliyetokea Atletico Madrid ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mwanzoni mwa msimu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ujanja wa magavana wenye kesi kuendelea kuhudumu

Montreal yadumisha rekodi ya kutoshindwa MLS hadi mechi...