Michezo

Renhe ya Timbe yaanza ligi kwa kipigo

March 4th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Beijing Renhe, ambayo imeajiri winga Mkenya Ayub Timbe, imeanza maisha kwenye Ligi Kuu ya Uchina kwa kupigwa 1-0 na Chongqing Lifan uwanjani Chongqing, Jumamosi.

Renhe, ambayo inanolewa na Mhispania Luis Garcia Plaza, imepoteza mchuano huu kupitia bao la mshambuliaji Kardec Alan. Mbrazil huyu alipachika penalti safi dakika ya 23.

Ni mechi ya sita mfululizo ambayo Renhe imemaliza bila ushindi dhidi ya Chongqing. Renhe ilinyakua tiketi ya kurejea kwenye Ligi Kuu baada ya kushinda Ligi ya Daraja ya Pili (Jia League) mwaka 2017. Ilitemwa kutoka Ligi Kuu mwisho wa msimu 2015.

Timbe hakuwa kikosini kwa sababu alijiunga na klabu ya Heilongjiang Lava Spring, ambayo inashiriki Ligi ya Daraja ya Pili, kwa mkopo hadi Desemba 31, 2018.

Mechi ijayo ya Renhe ni dhidi ya viongozi Tianjin Quanjian hapo Machi 10. Ligi ya Jia itaanza Machi 10 ambapo klabu mpya ya Timbe itakabana koo na Shenzhen mnamo Machi 11.