Rennes wapiga PSG breki kali katika kampeni za Ligue 1

Rennes wapiga PSG breki kali katika kampeni za Ligue 1

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) walipokezwa kichapo cha kwanza katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Jumapili baada ya Rennes kuwatandika 2-0 ugani Roazhon Park.

Rennes waliokuwa wakichezea katika uwanja wao wa nyumbani waliwekwa kifua mbele na fowadi Gaetan Laborde mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Iliwachukua Rennes sekunde chache pekee mwanzoni mwa kipindi cha pili kupachika wavuni bao la pili baada ya Flavien Tait kujaza kimiani krosi safi aliyoandaliwa na Laborde.

Ingawa PSG walijitahidi kufunga bao la kuwarejesha mchezoni, juhudi zao zilizaa nunge huku goli la Kylian Mbappe likataliwa na refa aliyetumia teknolojia ya VAR kubainisha kwamba alicheka na nyavu akiwa ameotea. Mbappe kwa sasa hajafunga bao katika mechi tano zilizopita kwenye mapambano yote.

Chini ya kocha Mauricio Pochettino, PSG walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara licha ya kujivunia huduma za washambuliaji matata zaidi duniani – Mbappe, Neymar Jr na Lionel Messi.

Ushindi wa Rennes uliwapaisha hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la Ligue 1 kwa alama12 sawa na Olympique Lyon na AS Monaco. Ingawa PSG wangali wanadhibiti kilele cha jedwali kwa pointi 24, azma yao ya kuendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mechi tisa za ufunguzi wa kampeni za Ligue 1 muhula huu ilipigwa breki kali. Rennes watavaana na Metz katika mchuano wao ujao ligini huku PSG wakitarajiwa kujinyanyua dhidi ya Angers kampeni za ligi kuu mbalimbali zitakaporejelewa baada ya pumziko linalopisha michuano ya kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

PSG walishuka dimbani kuvaana na Rennes wakijivunia ushindi katika mechi nne mfululizo – rekodi iliyowawezesha kufungua mapema pengo la alama sita kuliko nambari mbili Lens kileleni mwa jedwali. Mojawapo ya mechi zilizovunia PSG ufanisi huo ni ushindi wa 2-0 dhidi ya Manchester City kwenye kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku ugani Parc des Princes, Ufaransa.

Messi alitumia gozi hilo la UEFA kufungua rasmi akaunti yake ya mabao kambini mwa PSG waliomsajili mwanzoni mwa muhula huu kutoka Barcelona ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Kwa upande wao, Rennes walishuka ugani wakipania kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi katika mechi mbili za awali ligini.

Kikosi hicho kilikuwa pia na motisha ya kuendeleza makali yaliyokiwezesha kusajili uahindi wa kwanza katika Europa Conference League mnamo Alhamisi iliyopita baada ya kutoka nyuma na kutandika Vitesse ya Ligi Kuu ya Uholanzi 2-1.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Firat atatangaza kikosi cha Harambee Stars kusafiri Morocco...

FAO yahimiza vijana wawe mstari wa mbele katika shughuli za...