Michezo

Rhonex Kipruto atarajiwa kwenye Kip Keino Classic

September 30th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHINDI wa nidhani ya shaba katika mbio za mita 10,000 duniani, Rhonex Kipruto, atakuwa miongoni mwa wanariadha 97 watakaonogesha Riadha za Dunia za Mabara za Kipe Keino Classic uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Oktoba 3, 2020.

Kati ya vitengo vitakavyoshindaniwa kwenye Kip Keino Classic ni mbio za kilomita 20, kuruka juu (wanaume), kuruka mbali (wanawake), mita 4×400 kupokezana vijiti (wanawake na wanaume), mita 400 kuruka viunzi (wanaume) na mita 10,000 (wanaume).

Mbio za mita 10,000 zitakazoitwa “Naftali Temu 10,000m Classic, zinatarajiwa kuibua msisimko zaidi baada ya kuvutia jumla ya wanariadha 25.

Kurusha kisahani, mita 200, mita 3,000 kuruka viunzi na maji ni kategeoria nyinginezo zitakazoshirikisha wanawake na wanaume. Patakuwepo pia na urushaji mkuki (wanaume), mita 400, mita 800, mita 1,500 na mita 5,000 kwa wanawake na wanaume.

Paul Mutwii ambaye ni mkurugenzi wa mashindano kutoka Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), amesema kikosi kitakachopeperusha bendera ya taifa kiliteuliwa kwa misingi ya matokeo yao ya kitaifa mwaka jana (iwapo walitinga tatu-bora kwenye fani zao) na jinsi walivyofaulu kwenye makala yaliyopita ya Riadha za Dunia, Michezo ya Afrika na mapambano ya kitaifa.

Wengine waliteuliwa kutoka kwa asasi maalumu za serikali kama vile Kenya Police, Jeshi la Kenya (KDF) na Kenya Prisons (Magereza).

“Wanariadha wote watakaoshiriki watafanyiwa vipimo vya corona kufikia Ijumaa,” akasema Mutwii kwa kufichua kwamba mashindano ya kitaifa yatakayojumuisha vitengo vyote vya riadha kwa upande wa wanawake na wanaume yataandaliwa kabla ya mwaka huu kukamilika.

“Tulitarajia kupata wanariadha wa haiba kubwa zaidi katika vitengo vya mbio za masafa mafupi, kadri na marefu pia. Hata hivyo, wengi wameonekana kuvutiwa zaidi na mashindano ya uwanjani,” akatanguliza Mutwii.

 “Janga la corona pia limeathiri idadi kubwa ya wanariadha ambao wangenogesha mbio hizi. Wengi wao walifunga msimu baada ya kushiriki duru ya mwisho ya Diamond League jijini Doha, Qatar mnamo Septemba 25,” akasema Mutwii katika kauli iliyoungwa na kinara mwakilishi wa wanariadha wa ughaibuni katika Kip Keino Classic, Marco Corstjens.

Mwitaliano Marco Lingua, anayejivunia rekodi ya mita 79.97, Pavel Bareisha na Zakhar Makhrosenka wote kutoka Belarus, na Petr Koucky wa Jamhuri ya Czech watashiriki fani ya kurusha kijiwe ambayo pia itamjumuisha Mkenya Dominic Abunda.

Vanessa Sterckendries wa Ubelgiji, Valeriya Icanenko wa Ukraine na Amastasiya Kalamoeta (71.99) kutoka Belarus watanogesha kitengo cha urushaji wa kijiwe kwa upande wa wanawake.

Wengine ni Tracey Anderson wa Uswidi, Rosa Rodriguez (73.64m) wa Venezuela, Katerina Chlupova wa Jamhuri ya Czech na Mkenya Rebecca Kerubo.

Licha ya kujiondoa kwa mshindi wa nishani ya fedha katika Olimpiki na bingwa wa zamani wa dunia, Julius Yego katika urushaji wa mkuki, fanu hiyo bado inajivunia miamba mbalimbali.

Baadhi yao ni Johan Grobler (80.59m) kutoka Afrika Kusini na Hubert Chmielak (82.58m) wa Poland.

Wengine ni Mfaransa Lukas Moutarde, Sokola Dominik wa Jamhuri ya Czech na Timothy Herman wa Ubelgiji. Hawa watatoana jasho na Wakenya Alexander Kiprotich, Duncan Kinyanjui na Methusellah Kiprop.

Vita vya ubabe vilivyotarajiwa kati ya Conseslus Kipruto na mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Riadha za Dunia, Soufiane El Bakkali wa Morocco, huenda visikuwepo.

El Bakkali alipata jeraha wakati akishiriki mbio za mita 1,500 kwenye Doha Diamond League zilizomshuhudia Kipruto akijiondoa.

“Kipruto na El Bakkali wana majeraha. Ni matumaini yetu kwamba watapona upesi na kuwa tayari kwa mbio hizo,” akasema Corstjens.

Abraham Seme kutoka Ethiopia, Abel Sikowo wa Uganda na Hilal Yego kutoka Uturuki ni miongoni mwa wanariadha watakaoshirki mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji.

Mbio hizo zimewavutia pia Amos Kirui aliyeibuka bingwa wa dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mnamo 2016 na Leonard Bett aliyeibuka bingwa wa dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 mnamo 2018. Kirui pia aliibuka bingwa wa kitaifa katika mbio za nyika mnamo 2019.

Mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji vitamjumuisha Beatrice Chepkoech na Hyvin Kiyeng aliyeridhika na medali ya fedha katika Olimpiki za Rio 2016 nchini Brazil. Wawili hao watatoana jasho na wanariadha nyota kutoka Uganda, Ethiopia na Bahrain.

Bingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000 Edris Muktar, mshindi wa nishani ya fedha katika mbio za mita 5,000 duniani Selemon Barega na Hagos Gebrhiwet aliyejizolea medali ya fedha katika Olimpiki za 2016, hawatakuwa Nairobi kwa minajili ya mbio za mita 5,000 za Kip Keino Classic.

Muktar anauguza jeraja, naye Barega alifunga kampeni zake za msimu huu kwa kivumbi cha Doha Diamond League. Chipukizi Worku Tadese na Berihu Aregawi ambaye ni mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 10,000 duniani kwa chipukizi wa U-20, watawakilisha Morocco kwenye mbio hizo za mita 5,000.

Jacob Krop na Nicholas Kimeli aliyeambulia nafasi ya nane katika mbio za mita 5,000 jijini Doha wataongoza kikosi cha Kenya. Kimeli atapania kuendeleza ubabe uliomshuhudia akiibuka mshindi wa kivumbi cha Gouden Spike mjini Leiden, Norway kwa muda wa dakika 26:58.97 mnamo Septemba 19, 2020.