Michezo

Riadha: Kikosi cha taifa kuanza kujiandalia Doha

September 11th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

TIMU itakayowakilisha Kenya katika Riadha za Dunia jijini Doha, Qatar kati ya Septemba 27 na Oktoba 6, 2019, inatarajiwa kupiga kambi kwa mazoezi zaidi ya kujifua mnamo Jumapili wiki hii.

Kikosi kamili kitakachopeperusha bendera ya taifa kitafichuliwa rasmi mnamo Ijumaa, muda mfupi baada ya kukamilika kwa mchujo wa kitaifa utakaoendeshwa na Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) kuanzia kesho uwanjani Nyayo, Nairobi.

Kwa mujibu wa Barnabas Korir ambaye ni Mwanakamati Mkuu wa AK, mahali ambapo kikosi cha Kenya kitapigia kambi kabla ya kufunga safari ya kuelekea Qatar patajulikana pia mwishoni mwa mbio za mchujo.

“Serikali itatueleza mahali patakapowafaa wanariadha wetu kwa mazoezi ya wiki moja na nusu kabla ya Riadha za Dunia kuanza,” akasema kinara huyo.

Wanariadha watakaowakilisha Kenya katika marathon kwa upande wa wanaume na wanawake wanatarajiwa kuelekea Doha mnamo Septemba 24 kabla ya kikosi kingine kufunga safari siku moja baadaye.

Vikosi vya Kenya kwa minajili ya marathon na mbio za mita 10,000 kwa upande wa wanaume na wanawake tayari vimeteuliwa. Ni wanariadha watakaowania nishani katika fani nyinginezo ndio watakaojulikana mwishoni mwa mchujo wa Ijumaa.

Kenya itawakilishwa na wanariadha 46 jijini Doha. Kulingana na Korir, kati ya watimkaji hao, wote isipokuwa bingwa wa Afrika katika mbio za mita 5,000 Robert Kiprop wametimiza masharti na kanuni za Jopo la Maadili la Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) baada ya kufanyiwa ukaguzi wa kubaini iwapo wamewahi kutumia dawa za kusisimua misuli.

Ni matumaini ya Korir hata hivyo kwamba Kiprop atakuwa amefanyiwa ukaguzi huo kufikia siku ya kuondoka kwa kikosi cha Kenya humu nchini iwapo atakuwa miongoni mwa wataokamilisha mbio za mita 5,000 ndani ya mduara wa tatu-bora katika mchujo wa Alhamisi.

Nafasi tatu za kwanza

Mbali na wanariadha watakaoibuka kwenye nafasi tatu za kwanza katika kila fani mchujoni, mabingwa watetezi wa Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini London, Uingereza mnamo 2017 pia watajikatia tiketi za kuwakilisha Kenya jijini Doha.

Wengine watakaofuzu ni wanariadha wote waliohifadhi ubingwa wao katika kampeni za Diamond League msimu huu.

Elijah Manangoi (mita 1,500), Hellen Obiri (mita 5,000), Conseslus Kipruto (mita 3,000 kuruka maji na viunzi) na Faith Chepngetich Kipyegon (mita 1,500) ndio wanariadha watakaolenga kuhifadhi mataji waliyoyatwaa 2017 wakiwa jijini Doha kuanzia mwisho wa Septemba.

Timothy Cheruiyot ambaye amekuwa bingwa wa msimu huu katika mbio za mita 1,500 ndiye mwanariadha wa hivi karibuni zaidi kujikatia pia tiketi ya kuwakilisha Kenya nchini Qatar baada ya kuhifadhi taji la IAAF Diamond League jijini Brussels, Ubelgiji mwishoni mwa wiki iliyopita.

Watimkaji wengine watakaoelekezewa macho ya karibu katika fainali za mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanaume ni bingwa wa dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 (U-20), George Manangoi, Charles Simotwo, bingwa wa dunia kwa chipukizi wa U-20 mnamo 2015, Kumari Takin a Ronald Kwemoi aliyeibuka mfalme wa Afrika katika fani hiyo mnamo 2014.