Habari Mseto

RIBA: Korti yaiagiza Jamii Bora iilipe Vaell Sh8 milioni

December 31st, 2018 1 min read

NA FAUSTINE NGILA

KAMPUNI ya ukodishaji wa magari ya  Vehicle and Equipment  Leasing Limited (Vaell) imevuka mwaka kwa tabasamu baada ya mahakama kuu kuiamuru benki ya Jamii Bora iirudishie Sh8 milioni ambazo ni fedha za riba ya juu iliyolipisha  kampuni hiyo katika mkopo iliyochukua.

Kwenye maombi iliyowasilisha mbele ya Jaji James Makau katika mahakama kuu ya Milimani Desemba 20, Vaell ilitoa sababu kadha ikitaka uamuzi wa awali hapo Julai 2017 ubatilishwe, kwa kuwa ulikuwa na makosa.

“Ilibainika kuwa mshtakiwa alikuwa ameipotosha korti kwa kuamini kuwa riba iliyotozwa mlalamishi ilikuwa ya kweli, kwani haikufuata kifungu cha 33B cha Sheria ya Benki, na kumtoza mlalamishi riba ya juu zaidi,” ikasema taarifa ya hukumu.

Katika awamu ya kwanza ya kusikizwa kwa kesi, benki ya Jamii Bora haikutoa stakabadhi za malipo ya mkopo wa Vaell kortini, na hivyo ilikuwa vigumu kung’amua kiwango cha riba ilichotoza.

Katika barua iliyoandikia korti hapo Februari 2018, mshatikiwa alikiri kuwa alimtoza mlalamishi riba ya juu, badala ya kutoza asilimia 14 kulingana na sheria za utozaji riba nchini. Korti ilisema mshtakiwa alifanya hivyo kimakusudi.

Kwenye maombi yake, Vaell iliiomba korti iamrishe Jamii Bora iilipe Sh300 milioni kama fidia ya kupoteza mapato ya biashara, Sh181.8 milioni kama fidia baada ya kampuni ya Manara kupoteza wateja, Sh41.6 kama fidia baada ya kampuni ya Manara kufuta mkataba wa kibiashara, Sh16.5 milioni ilizotoza juu ya riba ya asilimia 14, Sh8 milioni kama riba ya juu baada ya sheria ya riba kubatilishwa na Sh3.7 milioni kama fidia ya Telkom na Sh3.6 milioni kama gharama za kibiashara.

Lakini kati ya maombi haya yote, kufikia sasa ni Sh8 milioni kama riba ya juu baada ya sheria ya riba kubatilishwa ambazo benki ya Jamii Bora imetakiwa kuilipa Vaell huku kesi ikiendelea.