Rift Valley yapata mshirikishi mpya

Rift Valley yapata mshirikishi mpya

Na CHARLES WASONGA

KAMISHNA wa kaunti ya Makueni Mohamed Maalim amepandishwa cheo baada ya kuteuliwa kuwa Mshirikishi mpya wa Kanda ya Rift Valley kuchukua nafasi ya George Natembeya aliyejiuzulu Jumatano, Januari 12, 2022.

Mabadiliko hayo yametangazwa Alhamisi na Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho.

Bw Natembeya ambaye amehudumu kama afisa wa utawala, tangu cheo cha mkuu wa tarafa (DO) alijiuzulu ili awanie ugavana wa Trans Nzoia katika uchaguzi mkuu ujao.

“Kuanzia leo sitakuwa mshirikishi wa Kanda ya Rift Valley. Mwenzangu atachukua nafasi yangu wiki hii au wiki ijayo. Kutoka hapa nitaelekea Nairobi kujiandaa kuchua likizo fupi kabla ya kuelekea Trans Nzoia kuitikia wito wa wananchi kuwahudumia kama gavana,” Bw Natembeya akawaambia wanahabari katika afisi ya Mshirikishi wa Kanda, jijini Nakuru.

Kulingana na sheria za uchaguzi, watumishi wa umma ambao wanataka kuwania nyadhifa za kisiasa sharti wajiuzulu miezi sita kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Kwa kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utafanyika Agosti 9, 2022 watumishi wa umma wanaopania kujitosa siasa wanahitajika kujiuzulu kufikia Februari 9, 2022.

Bw Natembeya anatarajiwa kupambana na Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa miongoni mwa wagombeaji wengine katika kinyang’anyiro cha kurithi kiti cha ugavana wa Trans Nzoia.

Gavana wa sasa Patrick Khaemba hatawania kwa kuwa anahudumu muhula wa pili na wa mwisho, kwa mujibu wa Katiba ya sasa.

Wakati huo huo, Bw Natembeya ameitwa Nairobi kwa shughuli ya kurejesha mali na stakabadhi zote za serikali.

You can share this post!

Jubilee ingali imara wala haijafa, adai Mbunge Kanini Kega

Dimba la 1-0 Nigeria wakiwavuruga Misri

T L