Habari za Kitaifa

Rigathi alinyimwa ndege? Naibu Rais alivyochelewa hafla ya Rais kwa zaidi ya saa nzima

June 10th, 2024 2 min read

NA ERIC MATARA

NAIBU wa Rais Rigathi Gachagua Jumapili alilazimika kuomba radhi kwa Rais William Ruto, baada ya kuwasili kuchelewa katika hafla ya kitaifa ya maombi ya dhehebu la Akorino katika Kaunti ya Nairobi.

Bw Gachagua alifika kwenye hafla hiyo iliyokuwa inafanyika katika uga wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Nakuru akiwa ameabiri helikopta ya kibinafsi, karibu saa nzima baada ya Rais na msafara wake kuwasili.

Naibu Rais ambaye alikuta hafla tayari inaendelea alilazimika kuomba radhi kwa Rais, wakati alipoitwa kuzungumza.

“Bw Rais, kwanza kabisa, nataka kuomba radhi kwa kufika kuchelewa. Mimi sifahamiki kwa utovu wa nidhamu. Unajua vizuri mimi nilikuwa afisa wa kuvalia sare na kwenye serikali yako, mimi ndiye niliye na nidhamu zaidi,” akasema Bw Gachagua.

“Nilikuwa na changamoto kwenye mipango yangu ya usafiri, na pia nilikumbana na matatizo ya hali ya anga kati ya Naivasha na Longonot kwa karibu saa nzima,” akaeleza Gachagua.

Rais Ruto alikuwa amewasili kwenye hafla mapema, akiwa ameabiri ndege ya kijeshi ya Airforce One na akalakiwa na wanasiasa wa eneo hilo, wakiongozwa na Gavana wa Nakuru Susan Kihika na Waziri wa Maji Zachary Njeru.

Haikufahamika mara moja kilichosababisha ‘matatizo’ ya usafiri ambayo Bw Gachagua alitaja yalimfanya kukawia katika safari yake ya Nakuru.

Lakini kuzungumzia waziwazi kwamba alikuwa na changamoto za usafiri kunaibua maswali mengi kuhusu hali yake ya maslahi katika serikali hiyo ambayo yeye ndiye wa pili kwa ukubwa na mamlaka.

Haya yanajiri karibu wiki moja tangu Waziri wa Ulinzi Aden Duale kupiga marufuku wanasiasa dhidi ya kutumia ndege za kijeshi.

Bw Duale ambaye alizungumza hayo wakati wa mahojiano katika kituo kimoja cha runinga, alisema hatua hiyo ilikuwa inaenda sambamba na kanuni mpya za KDF zinazolenga kuiepusha na matumizi mabaya ya rasilmali zake.

“Helikopta za KDF hazitaruhusiwa tena kutumiwa na wanasiasa. Ndege hizo na rasilmali zingine zitakuwa tu zinatumika kwa shughuli maalum za kijeshi ikiwemo kubeba wanajeshi na wakati wa operesheni maalum,” alisema Bw Duale.

Naibu Rais ni miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu ambao awali walikuwa wanatumia ndege za kijeshi kwa usafiri.

Wengine ambao wametumia ndege hizo ni Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na Bw Duale wakati wa kuzuru maeneo maalum ya kikazi.