Habari za Kitaifa

Riggy G kuwasilisha malalamishi dhidi ya Jaji ‘aliyemhangaisha’

January 15th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesema atawasilisha kesi kuishinikiza Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kumwondoa Jaji Esther Maina katika Idara ya Mahakama, kwa madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.

Akizungumza Jumapili, Januari 14, 2024 mjini Iten, Kaunti ya Elgeyo Marakwet, katika ibada ya kanisa iliyokuwa imehudhuriwa na Rais William Ruto, Bw Gachagua alisema Jaji Maina alitangaza kwamba alipata mali yake kwa njia haramu, bila ya kumpa nafasi yoyote kujitetea.

Bw Gachagua alisema kuwa atawasilisha malalamishi yake kwa JSC, Alhamisi (Januari 18, 2024), saa 8.15 alasiri.

“Alhamisi wiki ijayo, saa 8.15 alasiri, nitawasilisha malalamishi yangu binafsi mbele ya Jaji Mkuu Martha Koome dhidi ya Jaji Eshter Maina. Nitashinikiza aondolewe kutoka Idara ya Mahakama kwa ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka,” akasema Bw Gachagua.

Taarifa yake inafuatia hatua ya Bi Koome kuwaalika Wakenya wote kuwasilisha ushahidi wowote walio nao kuhusu majaji kujihusisha na ufisadi kwa JSC.

Kwenye hotuba yake Jumapili, Bw Gachagua alidai kwamba ana ushahidi unaomhusisha Jaji Maina na ufisadi.

“Kutokana na kesi iliyokuwa ikinikabili, tulituma ombi la kumhoji afisa aliyekuwa akinichunguza, lakini (Jaji Maina) akakataa kwani alifahamu hakukuwa na kesi yoyote,” akasema Bw Gachagua.

Bw Gachagua alikuwa akirejelea kesi ambapo Jaji Maina aliagiza akaunti yake (Gachagua) kufungwa mnamo Julai 2022.

Jaji huyo alimwagiza Bw Gachagua kuikabidhi serikali jumla ya Sh202 milioni, alizodai zilitokana na ufisadi.

Jaji huyo alisema kuwa Bw Gachagua alishindwa kueleza alivyopata pesa hizo.

Wakati huo, Bw Gachagua alikuwa akihudumu kama mbunge wa eneobunge la Mathira.

“Wakenya wenye malalamishi wanafaa kuyawasilisha. Ninawarai Wakenya wenye nia kuungana nami Alhamisi ili kuwasilisha malalamishi yao pia,” akasema Bw Gachagua.

Kesi hiyo ilitokana na akaunti tatu za Bw Gachagua, ambapo Mamlaka ya Kutwaa Mali (ARA) ilifanya uchuguzi wa kina kuhusu Sh7.3 bilioni zilizokuwa zimetumwa ama kutoka katika akaunti hizo.