Makala

Riggy G, mkewe wang’ang’ania shamba na afisa wa zamani hati mbili ‘halali’ zikiibuka

January 2nd, 2024 3 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MZOZO kuhusu ardhi ya hektari mbili ya thamani ya Sh1.5 bilioni inayong’ang’aniwa na kampuni ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na mkewe Dorcus na aliyekuwa afisa mkuu mstaafu wa wizara ya ardhi umechukua mwelekeo tofauti baada ya kuibuka kuwa kuna hati mbili halisi za umiliki.

Jaji Joseph Mboya sasa atalazimika kuamua iwapo shamba hili ni mali ya Wamunyoro Investments Limited (WIL) ama ni ya Bw John Michael Ohas na kampuni yake Columbus Two Thosand Limited.”

Akitoa ushahidi katika kesi ambapo kampuni ya Wamunyoro Investments Limited yake Bw Gachagua na mkewe Dorcus imemshtaki Bw Michael John Ohas, kampuni ya Columbus Two Thousand Limited na Msajili Mkuu wa Hatimiliki za Mashamba, mkurugenzi wa Ardhi Gordon Odeka Ochieng, alisema hati mbili halisi zilitayarishwa na kutiwa sahihi na Kamishna wa Ardhi.

Wamunyoro iliyowasilisha kesi hiyo 2022 inaomba mahakama kuu iitangaze mmiliki halisi wa shamba hilo na wala sio Columbus na Bw Ohas.

Alilitawisha 1994

Jaji Mboya alifahamishwa na Bw Ochieng, ambaye amehudumu katika wizara ya ardhi kwa miaka 34, kwamba Ohas alikabidhiwa shamba hilo na kulistawisha mwaka wa 1994 ilhali Wamunyoro ilikabidhiwa shamba hilo 2002.

Katika kesi hii Bw Ochieng alithibitisha kwamba hati hizi mbili ni halisi- ya Columbus na Wamunyoro ya Bw Gachagua. Mkurugenzi huyu alionyeshwa mbele ya Jaji Mboya na wakili wa Serikali Bw Allan Kamau hati hizo mbili kutoka Wizara ya Ardhi kisha akasema “zote ziko halisi. Ziko sawa.”

Mkurugenzi huyo wa masuala ya ardhi alieleza Jaji Mboya kwamba kampuni ya Wamunyoro iliuziwa shamba hilo na Bw Peter Nduati Mbugua, Pauline Muringe na Karandi Farms Limited.

Wamunyoro ilipewa hati ya umiliki shamba hilo nambari IR90923/1 mnamo Desemba 31,2002.

Pamoja na hayo Kamishna wa Ardhi pia alitayarisha ya pili ya umiliki wa shamba hilo na kuikabidhi kampuni ya Columbus.
Jaji Mboya alifahamishwa hati hizi mbili zimesababisha hali ya taharuki.

Akasema Bw Ochieng: “Hati hii ya Columbus Two Thousand nambari IR209/12077 imezua mtafaruku kwa vile inamaanisha shamba hili liko na wamiliki wawili halisi.”

Akitoa maoni yake kama mtaalamu wa masuala ya ardhi, Bw Ochieng alimlaumu Kamishna wa Ardhi akisema alikosea kutoa hati mbili za umiliki wa shamba hilo kwa watu wawili.”

Akimalizia ushahidi Bw Ochieng alimng’ata Kamishna wa ardhi kwa kusema : “haikufaa kuipa Columbus hati ya umiliki wa shamba hilo ilhali lilikuwa limeuziwa Wamunyoro na Peter Nduati, Pauline Muringe na Karandi Farm Limited waliokuwa wamepewa hati ya umiliki 1999.”

Hivyo basi alisema hati ya Columbus haipasi kutambuliwa licha ya kwamba iliuziwa shamba hilo na serikali 1994.

Ushahidi wa Ohas

Ushahidi uliowasilishwa na Bw Ohas ni kuwa aliomba apewe shamba hilo 1994 kustawisha viwanda.

Columbus ilitakiwa ilipe ada ya Sh863,400 katika muda wa 30 na ikishindwa serikali ingetwaa tena umiliki wake.
Jaji Mboya alifahamishwa Columbus ililipa Sh50,000 mnamo 1996 na ikapewa risiti rasmi.

Columbus ilichelewa kulipa kwa zaidi ya siku 30.

Serikali ilitwaa tena umiliki wa shamba hilo na kuwapa Karandi Farm Limited. Peter N. Mbugua na Pauline Muringe.

Wamunyoro inadai Ohas alipata hatimiliki ya shamba hilo Septemba 2019 kinyume cha sheria.

Wamunyoro ilishtaki Ohas , Columbus Julai 2022 ikiomba korti ifutilie mbali hatimiliki ya Columbus.

Jaji huyo alifahamishwa Wamunyoro ilinunua shamba hilo kutoka kwa Karandi, Mbugua na Muringe mnamo Juni 18, 2012 kwa bei ya Sh24 milioni.

Mnamo Juni 27, 2013 Wamunyoro ilikopa Sh150 milioni kutoka kwa benki ya Equity. Iliongeza mkopo mwingine wa Sh50 milioni.

Ahirishwa hadi mwaka huu

Jaji huyo aliahirisha kesi hiyo hadi mwaka huu.

Mbali na kesi hii inayosikizwa na Jaji Mboya mnamo Juni 16 2023 Polisi walimkamata Bw Ohas na wakili Moses Abongo Owuor na kumfungulia mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu wa mahakama ya Milimani Bw Lucas Onyina.

Lakini mnamo Juni 2023 walipofikishwa mbele ya Bw Onyina, mawakili Eric Theuri (rais wa chama cha mawikili nchini-LSK), Prof Elisha Ongoya na Apollo Mboya walipinga Bw Owuor na Bw Ohas wakisomewa na kujibu mashtaka kuhusu umiliki wa shamba hili la hektari mbili.

Mawakili hao waliteta vikali wakidai kukamatwa na kufikishwa kortini kwa wawili hao ilikuwa njama ya kusambaratisha kusikizwa kwa kesi kuhusu umiliki wa shamba hili katika Mahakama kuu Juni 2023.

Mawakili Theuri , Prof Ongoya na Mboya walisimama kidete na kumsihi Bw Onyina aahirishe kushtakiwa kwa Owuor na Ohas hadi kesi waliyoshtaki katika mahakama kuu isikizwe na kuamuliwa.

Bw Onyina alifahamisha Mboya kwamba Bw Owuor ni wakili anayemwakilisha Bw Ohas katika kesi ya umiliki wa shamba hilo inayoendelea katika mahakama kuu.

Hakimu alifahamishwa kesi hiyo ya mahakama kuu ilikuwa imeorodheshwa kusikizwa Juni 17,2023 ndipo wawili hao wangekamatwa na kufikishwa kortini Juni 16,2023 kwa lengo ya kusambaratisha kesi hiyo.

LSK iliwasilisha kesi katika mahakama kuu na kuomba kesi ya ulaghai wa shamba dhidi ya Owuor na Ohas isitishwe.
Bw Onyina alielezwa haki za Owuor na Ohas zilikandamizwa na polisi.

Kandamiza haki

Hakimu huyo aliombwa na mawakili hao asiruhusu mamlaka yake yatumiwe vibaya kukandamiza haki za Owuor na Ohas na Bw Gachagua akiwatumia polisi.

Bw Onyina alielezwa kuwa kampuni ya Bw Gachagua kwa jina Wamunyororo Investments Limited inadai umiliki wa shamba hilo.

Pia Bw Onyina alielezwa kampuni ya Columbus Two Thousand yake Bw Ohas ilipewa shamba hilo na kamishna wa ardhi.

Kufuatia ufichuzi huo Bw Onyina alisitisha kushtakiwa kwa wawili hao hadi pale mahakama kuu itakapotoa mwelekeo.

Na wakati huo huo Jaji Enock Chacha Mwita alisitisha kushtakiwa kwa Owuor na Ohas hadi Feburuari 6, 2024.