Kimataifa

Rihana alipwa mabilioni kutumbuiza wageni kwenye sherehe ya bwanyenye India

March 3rd, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MWANAMUZIKI Rihanna kutoka Amerika amelipwa Sh1.3 bilioni baada ya kutumbuiza wageni kwenye hafla ya matayarisho ya harusi ya mwanawe bwanyenye tajiri zaidi nchini India, Mukesh Ambani.

Mwanamuziki huyo alilipwa fedha hizo Ijumaa, Februari 2, 2024 baada ya kutumbuiza wageni mashuhuri waliohudhuria hafla ya Anant Ambani na mpenziye, Radhika Merchant.

Mukesh Ambani ni mfanyabiashara mashuhuri anayejishughulisha na utengenezaji na uuzaji dawa za matibabu.

Hafla hiyo ndiyo ilikuwa ya kwanza kwa mwanamuziki huyo mwaka huu, baada ya kuwatumbuiza mashabiki wake kwenye mashindano ya kitaifa ya kandanda ya kila mwaka nchini Amerika, Superbowl.

Hafla hiyo, ambayo ilianza Jumatano, iliendelea kwa siku tatu na imepangiwa kukamilika Jumapili, kulingana na vyombo vya habari nchini India.

Baadhi ya watu wengine maarufu ambao wamehudhuria hafla hiyo ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Meta (zamani Facebook), Mark Zuckerberg na mkewe Priscilla Chan.

Hafla hiyo inafanyika katika mji wa Jamnagar katika jimbo la Gujarat.

Anant, 28 amepangiwa kumwoa rasmi Radhika Julai 29.

Mamia ya wanakijiji pia walijumuika kwenye hafla hiyo.

Rihanna anafahamika kwa nyimbo maarufu kama ‘Umbrella’, ‘Unfaithful’, ‘Disturbia’ kati ya nyingine nyingi.

Licha ya kuishi Amerika, yeye ni mzaliwa wa Barbados.

Kulingana na jarida la Forbes, Rihanna ni miongoni mwa wanamuziki matajiri zaidi duniani.

Mwanaziki huyo pia anamiliki kampuni ya Fenty Beauty ambayo hutengeneza vipodozi vya wanawake.

Msanii huyo, 34, ana watoto wawili.