Rio Ferdinand amtaka Solskjaer abanduke Man-United kabla ya maji kuzidi unga

Rio Ferdinand amtaka Solskjaer abanduke Man-United kabla ya maji kuzidi unga

Na MASHIRIKA

MUSTAKABALI wa kocha Ole Gunnar Solskjaer kambini mwa Manchester United umetiliwa shaka na beki wa zamani wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Uingereza, Rio Ferdinand ambaye sasa amemtaka “ampishe mkufunzi mwingine”.

Solskjaer amekuwa katika presha kubwa ya kutimuliwa ugani Old Trafford tangu kikosi chake cha Man-United kikomolewe 5-0 na Liverpool kisha 2-0 na Manchester City katika kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Akizungumza katika kipindi chake cha YouTube cha ‘Vibe with Five’, Ferdinand alisema huu ndio wakati mwafaka zaidi kwa Solskjaer kubanduka Man-United kwa kuwa “ataondoka akiwa na hadhi pamoja na kitu cha kujivunia”.

“Kuanzia alikotutoa kama kikosi hadi tulipokuwa mwanzoni mwa msimu huu, nadhani Solskjaer alifanya kazi ya kuridhisha mno,” akatanguliza. “Lakini mahali tulipo kwa sasa si pazuri. Itakuwa vyema akiondoka kwa heshima badala ya kusubiri kutimuliwa wakati ambapo mazuri yote ambayo amefanyia klabu yatakuwa yameyeushwa na msururu wa matokeo duni,” akaongeza Ferdinand.

Man-City walipokeza Man-United kichapo cha 2-0 siku 13 baada ya masogora wa Solskjaer kupondwa 5-0 na Liverpool ugani Old Trafford. Man-United wamejizolea alama nne pekee kutokana na mechi sita zilizopita ligini na sasa wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 17, tisa nyuma ya Chelsea wanaoselelea kileleni.

Ferdinand, 43, alichezea Man-United kwa kipindi cha miaka 12 na kuzolea kikosi hicho mataji sita ya EPL.

You can share this post!

Uchovu walemaza kampeni za OKA

#KUMEKUCHA: Mwandishi wa Taifa Leo Wangu Kanuri aorodhesha...

T L