RIPOTI MAALUM: Echesa taabani kuagiza picha zake za ngono ziwekwe sura ya Malala

RIPOTI MAALUM: Echesa taabani kuagiza picha zake za ngono ziwekwe sura ya Malala

Na CHARLES WASONGA

VITA vya kisiasa baina ya Waziri wa Michezo Rashid Echesa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala sasa vimechukua mkondo mpya baada ya kuibuka madai kuwa waziri huyo alimhusisha seneta huyo na picha feki za ngono.

Seneta huyo wa chama cha ANC Jumatano aliwaambia wanahabari katika majengo ya bunge kwamba Bw Echesa, kwa ushirikiano na wanahabari fulani, walisambaza picha hizo mitandaoni zinazoonyesha Bw Malala akila uroda na kimada wakiwa uchi wa mnyama.

“Katika mitandao fulani ya kijamii kulisambazwa picha fulani za aibu zilizomwenyesha waziri akisema ndani ya danguro fulani na mwanamke wakiwa uchi. Picha hicho ziliposambaa, Rashid aliwatafuta wanahabari ambao aliwatumia hizo picha na akawaambia wazivuruge na kuweka sura yangu kisha wazisambaze,’ Bw Malala akasema.

“Lakini kwa sababu mimi nina mitandao ya kijasusi ikizingatiwa kuwa tuko serikalini, niliweza kuwasaka na kuwakamata wanahabari kwa usaidizi wa polisi,” seneta huyo akaongeza.

Bw Malala alisema Bw Echesa alilenga kutumia picha hizo kuendesha kampeni ya kumharibia jina.

 

Kuchafuliwa jina

“Lengo kuu la kitendo hichi cha aibu ni kueneza picha hizo chafu mitandaoni ili kupaka tope jina langu miongoni mwa Wakenya, haswa watu watu wa Kakamega ambao walinipa wajibu wa kuwatumikia,” akasema Bw Malala.

“Aliwatumia wanahabari kwa jina, David Ndolo, Stafford Ondego na Alex Njue kutekeleza kitendo hichi cha aibu kisha kuisambaza kwa mitandao ya kijamii kuniharibia jina,” akaongeza, akisema walitwaa simu zao na kipatakalishi ambacho walikuwa wakitumia.

“Hii ni aibu ikizingatiwa kuwa kando na kuwa kiongozi, nina mke na watoto ambao bila shaka kitendo hichi hakijawafurahisha,” Bw Malala akaeleza huku akionekana mwenye hamaki.

Cleopa Malala aonyesha kipakatalishi kilichotumiwa na wanahabari kuhariri picha za ngono za Waziri Rashid Echesa na kuweka sura yake Oktoba 24, 2018. Picha/ Cgharles Wasonga

Mwanasiasa huyo, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Wachache katika Seneti, alihimili madai yake kwa kuwaonyesha wanahabari jumbe za simu na kwenye mtandao wa WhatsApp zikionyesha mawasiliano kati ya Waziri Echesa na wanahabari hao.

Kulingana na jumbe hizo, Waziri Echesa aliwatumia wanahabari hao Sh5,000 kupitia dereva wake kwa jina Fredrick Ouma, almaarufu Adamu.

“Na sekunde chache baada ya Ndolo kumtumia Echesa picha hizo zilizokarabatiwa, alizituma kwangu. Kwa hivyo, mimi ni shahidi katika kesi hii,” Malala akasema.

 

Ushahidi wahifadhiwa

Alisema amemwagiza wakili wake James Orengo kushirikiana na wataalamu wa kimtandao kuhifadhi ushahidi huu ili kuutumia kumfungulia mashtaka Waziri Echesa.

Alipoulizwa kuhusu chanzo cha hayo yote, Bw Malala akajibu hivi:

“Kuna malumbano tuko nayo na CS Rashid. Juzi alihojiwa katika radio mmoja ya lugha ya kinyumbani akasema mambo mengi sana ambayo sitaki kuyataja hapa kwa sababu yalilenga kuniharibia jina.

“Bw Malala alisema kuwa juzi Bw Echesa alimpigia simu akiuliza ni kwa nini nilimrejelea Naibu Rais William Ruto kama mtu mfisadi katika mkutano fulani wa kisiasa.

“Lakini nikamjibu kwamba nilikuwa nikinukuu ripoti ya hivi majuzi ya Shirika la Ipsos ambayo ilimworodhesha naibu rais kama miongoni mwa watu fisadi nchini.”

Waziri Echesa hakupatikana kutoa kauli yake kuhusu sakata hii kwa sababu simu yake ilikuwa imezimwa kuanzia wakati huo hali tulipokwenda mitamboni.

 

Ruto alimjengea Malala nyumba?

Wiki iliyopita Waziri Echesa alimsuta Bw Malala kwa kudai Naibu Rais Ruto kuwa “mwizi” ilhali ni kiongozi huyo aliyemjengea (Malala) nyumba nyumbani kwao kaunti ya Kakamega.

Waziri Echesa ambaye ni mtetezi wa Naibu Rais William Ruto sasa yuko taabani. Picha/ Maktaba

Kwenye mahojiano katika redio moja, Echesa anadai kuwa ni yeye alimtambulisha Malala kwa Ruto, wakati huo akiwa diwani, na akafadhili ujenzi wa nyumba yake (Malala) uliogharimu Sh7 milioni.

“Leo  hii, hana aibu akimwita mwanamume ambaye alimpa nyumba za kujengea nyumba yake ambako analea watoto wake, kuwa mwizi. Anaambia makanisa yakatae pesa za Naibu Rais. Nampa changamoto abomoe nyumba hiyo iliwa ilijengwa kwa pesa za wizi,” Echesa akasma kwenye mahojiano katika redio hiyo inyopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Kiluhya.

Kulingana na Sheria kuhusu matumizi mabaya ya Tarakilishi na Uhalifu wa Kimtandao iliyopitishwa Mei mwaka huu, mtu yeyote ambaye atapatikana na hatia ya kusambaza jumbe za uwongo atatozwa faini ya Sh5 milioni, au kifungo cha miaka 10, au adhabu zote mbili.

Usambazaji wa picha chafu zinazoonyesha uchi wa mwanadamu kupitia mitandao ya kijamii ni hatia ambayo adhabu yake ni faini ya Sh300,000 au kifungo cha jela cha miaka 30 au adhabu zote mbili.

You can share this post!

SAKATA YA MAHINDI: Serikali ilivyopoteza mabilioni

DIMBA PATRIOTS: Vipaji vya soka mtaani Kangemi

adminleo