Habari Mseto

Ripoti mpya zaibuka kuhusu Mwitaliano aliyetekwa nyara

August 10th, 2019 1 min read

Na CHARLES LWANGA

PIKIPIKI mbili zilizotumiwa kumteka nyara mhudumu wa kujitolea, Mwitaliano Silvia Romano eneo la Chakama, Kaunti ya Kilifi mnamo Novemba 2018 zilinunuliwa mjini Malindi siku tatu kabla ya kisa hicho, mahakama imeelezwa.

Mfanyabiashara John Karani aliyeuza pikipiki hizo, alieleza Hakimu Mkuu mjini Malindi Julie Oseko kwamba aliuza pikipiki moja kwa Sh40,000 na nyingine kwa Sh35,000 kwa Bw Said Adan Abdi, mmoja wa washukiwa watatu wakuu ambaye amewekewa kiasi cha Sh1 milioni kama zawadi kwa yeyote atakayesaida kukamatwa kwake.

Bw Karani, hata hivyo aliifafanulia korti alipokuwa akihojiwa na wakili Tonia Mwania, kwamba hakufahamu kuwa Bw Abdi alinuia kutumia pikipiki hizo kumteka nyara mhudumu huyo raia wa Italy.

Alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ambapo Bw Moses Luwali na Bw Adulla Gababa Wario wameshtakiwa kwa kumteka nyara Bi Romano mnamo Novemba 20, 2018.