Kimataifa

Ripoti: Wakenya wasema heri Amerika kuliko Uchina

October 3rd, 2018 1 min read

Na VALENTINE OBARA

WAKENYA wengi wangependa Amerika iendelee kuwa taifa lenye ushawishi mkubwa zaidi ulimwenguni kuliko Uchina, ripoti inaonyesha.

Ripoti ya utafiti wa shirika la Pew Research Center iliyotolewa Jumatano, inasema kuwa ni asilimia 13 pekee ya Wakenya ambao wangefurahi kama Uchina ingekuwa taifa lenye ushawishi mkubwa zaidi ulimwenguni.

Kwa upande mwingine, asilimia 65 ya wananchi walipoulizwa wangependa taifa lipi liwe kuu ulimwenguni, walitaja Amerika.

‘Matokeo yanaonyesha kwamba kwa jumla, Amerika inapendwa zaidi. Amerika ilitajwa sana kuliku Uchina katika kila nchi ambapo utafiti huu ulifanywa isipokuwa Argentina, Tunisia na Urusi ingawa kuna pia nchi nyingi ambapo waliohojiwa walisema itakuwa vyema kama mataifa hayo mawili yatakuwa na ushawishi mkubwa kwa pamoja ulimwenguni,’ ripoti hiyo inaeleza.

Miongoni mwa masuala yaliyofanya Wakenya wengi kupenda Amerika kuliko Uchina ni kwamba wanaamini taifa hilo huzingatia sana maslahi ya Kenya wakati linapopitisha sera zake.

Utafiti huo ulifanywa wakati ambapo Uchina inazidi kupenyeza nchini humu kwa uwekezaji katika miradi mikubwa ikiwemo reli mpya ya SGR na barabara kuu kadhaa.

Wengi hulaumu Uchina kwa kushawishi serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kuchukua madeni makubwa ambayo yanalaumiwa kwa gharama kubwa ya hali ya maisha inayokumba wananchi hivi sasa.

Mbali na ripoti hiyo kuonyesha Wakenya wengi wako radhi kuona Amerika ikizidi kuongoza kiushawishi ulimwenguni kuliko Uchina, ilibainika kuwa idadi kubwa wana imani zaidi kwa Rais Donald Trump wa Amerika (asilimia 56) kuliko mwenzake wa Uchina Xi Jinping (asilimia 53).

Ingawa Wakenya wengi, sawa na raia wengi wa mataifa mengine walibainika kukubali kwamba majukumu ya Uchina ulimwenguni yameongezeka kwa mwongo mmoja uliopita, wengi walisema hilo halimaanishi kwamba ni jambo jema.