Habari

Ripoti ya BBI yazua joto kabla itolewe

October 25th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE na DAVID MWERE

WANASIASA wameanza kupiga kampeni kuhusu ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) hata kabla haijawasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Wabunge 39 wa chama cha Jubilee kutoka Mlima Kenya, walisema Alhamisi wataunga mkono ripoti hiyo iwapo tu itajumuisha mapendekezo kuhusu usawa katika uwakilishi kulingana na idadi ya watu pamoja na ugawaji wa rasilimali za kitaifa.

Kwenye taarifa ya pamoja waliyotoa katika majengo ya bunge jijini Nairobi, wabunge hao wakiongozwa na maseneta Mithika Linturi (Meru), Isaac Mwaura (Seneta wa Kuteuliwa) na Mbunge wa Ndaragwa, Jeremiah Kioni, lengo lao kuu ni haki kwa eneo la Mlima Kenya.

“Tunataka kusema masharti yetu ni kwamba lazima hitaji la usawa wa kijamii lizingatie uongozi, uwakilishi, ugavi wa rasilimali na muundo wa utawala,” akasema Bw Kioni aliyesoma taarifa kwa niaba ya wenzake.

Katika Kaunti ya Murang’a, viongozi wanaoegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta nao walianza mikutano ya kupigia debe ripoti hiyo inayotarajiwa kutolewa Rais Kenyatta atakaporudi nchini kutoka Urusi.

Viongozi hao waliojumuisha wabunge wa zamani na maafisa wa zamani wa chama kilichokuwepo cha TNA, walifanya mkutano wa faragha na viongozi wa kijamii wapatao 100 mjini Kenol kwa karibu saa tano.

Aliyekuwa Mbunge wa Kangema, Bw Tirus Ngahu alisema mkutano huo ulikuwa wa kupanga mikakati kuhusu utekelezaji wa ripoti ya BBI.

“Nchi lazima ifanyie katiba marekebisho na hili lilionekana wazi kutokana na mapendekezo yaliyowasilishwa kwa jopo la maridhiano lilipozuru kaunti zofauti,” akasema Bw Ngahu.

Kupinga

Mnamo Jumatano katika eneo la Sekenani lililoko eneobunge la Narok Magharibi, Kaunti ya Narok, viongozi kadhaa wa Jubilee walioandamana na Naibu Rais William Ruto, walisema watapinga ripoti ya BBI kama itatoa mapendekezo yatakayojali masilahi ya wanasiasa bila kunufaisha wananchi.

Viongozi hao walijumuisha Gavana wa Narok Samuel Tunai na wabunge Gabriel Tongoyo (Narok Magharibi), Johana Ng’eno (Emurua Dikirr), Soipan Tuya (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Narok), Caleb Kositany (Soy) na Nelson Koech (Belgut).