Makala

Ripoti ya 'Production Gap' yapendekeza mataifa yapunguze matumizi ya nishati ya visukuku

December 2nd, 2020 4 min read

Na MWANDISHI WETU

NI sharti serikali ulimwenguni zipunguze uzalishaji wa nishati ya visikuku kwa asilimia 6 kwa mwaka ili kupunguza hali hatari ya ongezeko la joto

Makala ya kipekee ya Ripoti ya ‘Production Gap’ ya mwaka 2020 kutoka kwa mashirika makuu ya utafiti na Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa kujiimarisha baada ya COVID-19 ni fursa mzuri kwa nchi mbalimbali, ikisema ipo haja ya kubadili mienendo ili kudhibiti viwango vya joto wakati wa uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi na kuvidhibiti visizidi nyuzijoto 1.5.

Ripoti hiyo, inaelezea masikitiko kwamba nchi zinapanga kuongeza uzalishaji wa nishati ya visukuku kwenye mwongo ujao licha ya utafiti kuonyesha kuwa ulimwengu unahitaji kupunguza uzalishaji wake kwa asilimia sita kwa mwaka ili kudhibiti ongezeko la joto duniani.

Ripoti hii iliyozinduliwa mara ya kwanza katika mwaka wa 2019, inapima pengo kati ya malengo ya Mkataba wa Paris na uzalishaji unaonuiwa kutekelezwa na nchi wa makaa ya mawe, mafuta na gesi.

Hii ina maana kuwa pengo la “production gap” linasalia kuwa kubwa kwa sababu nchi zinapanga kuongeza uzalishaji wa nishati ya visukuku zaidi ya maradufu katika mwaka wa 2030.

Makala ya kipekee yaliyotolewa mwaka huu yanaangazia athari za jangaa la COVID-19 – na mipango na mikakati ya serikali ya kujiimarisha na kuboresha uchumi– kuhusiana na uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi. Inatolewa wakati mwafaka ambao mabadiliko yanahitajika, kwa sababu janga hili linahitaji hatua za dharura kutoka kwa serikali – na wakati ambapo chumi kuu ikijumuisha China, Japan na Korea Kusini, zimetoa ahadi za kutozalisha gesi chafuzi kabisa.

“Mioto ya ajabu kutokea kwenye misitu, mafuriko, kiangazi na majanga mengine mabaya kutokana na hali ya hewa, ni ukumbusho tosha wa kwa nini tunahitaji kufaulu kukabiliana na majanga kwa mazingira,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Inger Andersen,.

Akaongeza: “Tunapojiandaa kuimarisha chumi baada ya jangaa la corona, kuwekeza kwenye nishati inayozalisha kiwango kidogo cha gesi ya ukaa na kwenye miundomsingi ina manufaa kwa chumi, kwa afya na kwa hewa safi. Ni sharti serikali zichukue fursa hii kwa kuhakikisha chumi na mifumo yake ya nishati inaacha kutumia nishati ya visukuku, na kujiimarisha vyema ili kuwa na mustakabali endelevu, wenye haki na ulio dhabiti.”

Ripoti yenyewe ilitolewa na Taasisi ya Mazingira ya Stockholm (SEI), Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (IISD), Taasisi ya Maendeleo Nje ya Nchi, E3G, na UNEP baada ya watafiti mbalimbali kutoka katika vyuo mbalimbali na mashirika mengine ya utafiti kushiriki kwenye uchanganuzi na uhariri.

Mwandishi mkuu wa ripoti hii na Mkurugenzi wa Kituo cha Amerika cha SEI Michael Lazarus alisema utafiti huo unaonyesha wazi kuwa kuna athari mbaya kwa mazingira iwapo nchi zitaendelea kuzalisha nishati ya visukuku kwa viwango vilivyopo, bila kuzingatia mipango yao ya kuongeza.

“Utafiti unatoa masuhuhisho kwa njia ya wazi: sera za serikali zinazopunguza mahitaji na usambasaji wa nishati ya visukuku na kusaidia jamii zinazovitegemea. Ripoti hii inatoa hatua ambazo serikali zinawezachukua kwa sasa ili kuwa na mabadiliko ya haki na yenye usawa bila kutumia nishati ya visukuku,” akasema Lazarus.

Kwanza, matokeo makuu ya utafiti huo yanajumuisha yanadhihirisha ili kuhakikisha joto linasalia kuwa la wastani nyuzijoto 1.5 dunia itahitaji kupunguza uzalishaji wa nishati ya visukuku kwa takribani asilimia sita kwa mwaka kati ya mwaka wa 2020 na mwaka wa 2030. Hata hivyo, watafiti wanasikitika kwamba nchi zinapanga na kunuia kuongeza viwango angalau kwa asilimia mbili kwa mwaka, hali ambayo kufikia mwaka wa 2030 itakuwa zaidi ya maradufu ua viwango inavyopaswa ili kutoziti nyuzijoto 1.5.

Pili, ripoti hiyo inasema kati ya mwaka wa 2020 na mwaka wa 2030, uzalishaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi duniani ni sharti upungue kwa asilimia 11, asilimia nne, na asilimia tatu, mtawalia ili kufanya joto kutozidi nyuzijoto 1.5.

Suala la tatu, ripoti inasema janga la COVID-19 – na masharti ya “kutotoka nje” ili kupunguza maambukizi – vimesababisha kupungua kwa uzalishaji wa nishati ya visukuku kwa muda katika mwaka wa 2020. Lakini mipango ya kabla ya corona na hatua za kujiimarisha baada ya corona ni ishara ya pengo linaloongezeka la uzalishaji wa nishati ya visukuku duniani, na kuhatarisha mazingira vibaya.

Jambo la nne ni kwamba kufikia sasa, serikali za G20 zimeahidi zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 230 kutumiwa kukabiliana na corona kwa sekta zinazoshughulika na uzalishaji na matumizi ya nishati ya visukuku duniani, pesa zaidi kuliko zile zinazotolewa kwa wanaotumia nishati isiyochafua mazingira (takribani dola za Kimarekani bilioni 150). Waundasera ni sharti wakabiliane na mwenendo huu ili kufikia malengo ya mazingira.

“Hali ngumu iliyosababishwa na ongezeko la bei ya mafuta mwaka huu pia inaonyesha kuwa maeneo na jamii zinazotegemea nishati ya visukuku ziko hatarini. Njia pekee ya kuepukana na mtego huu ni kuwa na uchumi anuai usiotegemea tu nishati ya visukuku. Ajabu ni kuwa katika mwaka wa 2020 tulishuhudia serikali nyingi zikiongeza maradufu nishati ya visukuku na kuongeza hatari zilizopo,” alisema Ivetta Gerasimchuk, mwandishi mkuu wa ripoti anayesimamia usambasaji wa nishati endelevu kwenye IISD.

“Badala yake, serikali zinapaswa kuelekeza fedha za kujiimarisha baada ya korona kuwezesha kuwa na chumi zanazotegemea vitu mbalimbali na kuanza kutumia nishati isiyochafua mazingira iliyo na manufaa ya kipindi kirefu kwa chumi na kwa ajira. Hii inaweza kuwa changamoto kuu katika karne ya 21, lakini ni muhimu na inaweza kutekelezeka.”

Ripoti hiyo pia inaonyesha jinsi ulimwengu unavyoweza kuacha kutumia nishati ya visukuku kwa njia iliyo na usawa, huku juhudi kubwa zikitarajiwa kutoka nchi tajiri zilizo na taasisi zenye uwezo wa kufanya hivyo na hazitegemei mno uzalishaji wa nishati ya visukuku. Baadhi ya wazalishaji wakubwa wa nishati ya visukuku kwenye kundi hili, ni pamoja na Australia, Canada na Amerika, na ni miongoni mwa nchi zinazotaka kuongeza usambasaji wa nishati ya visukuku.

Nchi ambazo zinategemea mno nishati ya visukuku na hazina uwezo wa kujimudu zitahitaji msaada wa kimataifa ili kuleta mabadiliko kwa njia iliyo na usawa, ripoti hiyo pia inaonyesha njia zinazoweza kutumika.

Watafiti wanahimiza ushirikiano ili dunia iondokane na kadhia hii.