Habari Mseto

Ripoti ya ukaguzi yabashiri kuporomoka kwa ODM bila Raila

May 9th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha ODM kimeanzisha juhudi za kujiimarisha upya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 baada ya ripoti ya uchunguzi kubaini kuwa huenda chama hicho kikasambaratika endapo kiongozi wake Raila Odinga hatakuwepo.

Mwenyekiti wa Kitaifa, John Mbadi, Jumatano aliungama kuwa japo chama hicho kinakabiliwa na changamoto za hapa na pale, hasa nyakati za mchujo, ki mbioni kukabiliana nazo.

Kulingana na ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la ODM Jumatatu, chama hicho kinamtegemea Bw Odinga zaidi hivi kwamba endapo hatakuwepo kitaporomoka.

“Walioandaa ripoti hiyo walifanya kazi nzuri. Inasheheni maoni ya viongozi na wafuasi wa chama chetu. Sasa sisi  kama uongozi wa chama tutaandaa mkutano wa kuchambua ripoti hiyo na kuratibu namna ya kutekeleza mapendekezo yake,” akasema Bw Mbadi.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kwamba chama hicho kifanye mageuzi katika asasi za uongozi wa chama hicho kabla ya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Shida zinayokumba chama chetu ni sawa na zile ambazo hukumba vyama vingine. Kwamba Bw Odinga ni kiongozi wetu haimaanishi kuwa chama kinamtegemea, bali yeye ni kiunganishi. Hali kama hii inashuhudiwa katika Jubilee chini ya uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta, Kanu kina Gideon Moi, ANC kina Musalia Mudavadi na vyama vinginevyo,” akasema Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini.

“Tutashughulikia masuala yote yaliyoibuliwa kwenye safu ya mapendekezo kwenye ripoti hiyo,” akaongeza mbunge huyo ambaye pia ni kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa.

Aidha, ripoti hiyo iliyowasilishwa katika kikao cha NEC kilichoongozwa na Bw Odinga, inaongeza kuwa ushawishi wa ODM umeshuka kutokana na utendakazi mbaya wa afisi kuu na Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama hicho nyakati za uchaguzi mkuu.

Ni kutokana na hali hiyo ambapo ripoti hiyo imeorodhesha msururu wa njia za kuimarisha sera za chama hicho pamoja na kanuni za kuendesha mchujo na chaguzi za mashinani.

Jopo kazi lililoendesha uchunguzi huo lilibuniwa mwaka 2018 chini ya uongozi wa Bi Catherine Muma. Wanachama wengine walikuwa Mwenyekiti wa NEB Judy Pareno, Mbunge wa Nyando Jared Okello, Afisa Mkuu Mtendaji wa ODM Oduor Ong’wen.

Wanachama wa jopo hilo wakishirikiana na maafisa wa kitaifa wa chama hicho watachambua ripoti hiyo kabla ya kuwasilisha ripoti katika mkutano wa NEC utakaofanyika Juni 2019.

Bw Odinga ana ushawishi mkubwa miongoni mwa wafuasi wa chama hicho kilichobuniwa baada ya kura ya maamuzi ya 2005. Baaadaye chama hicho kiliipa PNU ushindani mkubwa katika uchaguzi mkuu wa 2007.

Gavana wa Mombasa, Hassan Joho na mwenzake wa Kakamega Wycliffe Oparanya ndio manaibu wa Bw Odinga na kila mmoja anapania kurithi nafasi yake atakapostaafu siasa. Wawili hao wametangaza kuwa watawania urais mwaka 2022.