Habari

Ripoti yaanika uozo katika bima ya kitaifa ya afya NHIF

February 15th, 2020 2 min read

NASIBO KABALE NA SAMWEL OWINO

MATUMIZI mabaya wa fedha za umma, ulaghai, matumizi mabaya ya mamlaka na ufisadi ni miongoni mwa sababu ambazo zinadunisha huduma zinazotolewa na Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) kwa wateja wake.

Kulingana na ripoti iliyotayarishwa na Kundi la Wataalamu kuhusu Ufadhili wa Mageuzi katika Sekta ya Afya (Hefrep), hazina hiyo inakumbwa na matatizo kadhaa ya kiutendakazi ambayo yanaathiri huduma zake.

“Mpangilio wa sasa haushughulikii huduma zote ambazo zinahitajika kuifanya hazina hii kuwa mahsusi katika utendakazi wake. Pili, mpangilio huo umefanya majukumu yake kuhitilafiana pakubwa. Kutokana na hayo, idara mbalimbali za hazina hiyo huwa zinatekeleza majukumu yake bila mpangilio maalum wala mawasiliano yafaayo. Hilo linachangia pakubwa kudorora kwa huduma inazotoa,” inaeleza ripoti hiyo.

Hali hiyo pia imechangiwa pakubwa na ukosefu wa Afisa Mkuu Mtendaji tangu mwaka 2018, baada ya aliyekuwa msimamizi wake mkuu, Bw Geoffrey Mwangi na Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji Wilbert Kurgat kupewa likizo ya lazima, ili kutoa nafasi kwa uchunguzi kuhusiana na kupotea kwa mabilioni ya pesa.

Bw Nicodemus Odongo, ambaye amekuwa akihudumu kama Kaimu Mkurugenzi wa Mikakati, Mipango na Uuzaji, hakutuma ombi la nafasi ya Afisa Mkuu Mtendaji.

Meneja mmoja katika hazina hiyo ambaye hakutaka kutajwa, aliiambia Taifa Jumapili kwamba Waziri wa Afya, Bi Sicily Kariuki amekuwa akikataa majina ya watu wanaowasilishwa kwake na bodi bila kutoa sababu zozote.

“Nafasi hiyo ilitangazwa kuwa wazi mnamo Julai 2019. Hata hivyo, hakuna mtu aliyeteuliwa kuijaza. Kukataliwa kwa majina yanayowasilishwa ni ishara kamili kwamba kuna watu wenye ushawishi wanaomtaka mtu fulani atakayekuwa akifuata maagizo yao,” akasema.

Na licha ya kukamatwa kwa maafisa hao wawili na wafanyakazi wengine, hazina hiyo haijaondoa dhana ya kuwa fisadi.

Kwa mfano, mnamo Novemba 2019 Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) iliitaja kama taasisi fisadi zaidi nchini. Ilifuatwa na Kampuni ya Umeme (KP) na Idara ya Polisi.

Ripoti hiyo pia imeeleza kuhusu njia ambazo hazina huwa inapoteza fedha.