Habari

Ripoti yadai propaganda za Rogo zilieneza ugaidi

November 28th, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

USHAWISHI na mafunzo ya ugaidi yaliyokuwa yanaendeshwa na mwalimu mtatanishi wa dini ya Kiislamu, Sheikh Aboud Rogo, yameripotiwa kuharibu maisha ya mamia ya vijana nchini Kenya na mataifa mengine ya Afrika.

Imeibuka kuwa propaganda za kidini za Sheikh Rogo ndizo zimechangia uvamizi wa magaidi kaskazini mwa Msumbiji na Afrika Mashiriki.

Kulingana na ripoti ya msomi na mtafiti Ngala Chome ya ‘Eastern Africa’s Regional Extremist Threat: Origins, Nature and Policy Options’ ambayo ilitolewa Septemba 2020 ushawishi wa Sheikh Rogo ulisambaa katika nchi za Kenya hadi Tanzania na sasa unaendelea kuwa tishio kubwa katika nchi ya Msumbiji.

Ripoti hiyo ambayo imechapishwa na shirika la Centre for Human Rights and Policy Studies imefichua kuwa mawaidha ya itikadi kali za Sheikh Rogo yalienea na kuteka vijana wengi ambao sasa ni miongoni mwa wale ambao wapo nchini Msumbiji ambapo mashambulizi ya kigaidi yameendelea kushuhudiwa katika mkoa wa Cabo Delgado.

Kuchipuka kwa Sheikh Rogo, Bw Ngala anaeleza kwenye ripoti hiyo, kulitokana na hatua ya serikali kukataa kukisajili chama cha Waislamu nchini Kenya (IPK), mwaka 1990 hatua ambayo ilileta rabsha jijini Mombasa.

Baada ya kuchipuka kwa rabsha hizo, taarifa zinaeleza kuwa kikundi kilichokuwa kwenye chama hicho cha IPK kilianza kusambaza masomo ya itikadi kali na kuanza kupata ufuasi.

“Katikati ya mwaka wa 1990, wanachama wengi wa IPK miongoni mwao Sheikh Aboud Rogo Mohamed, Abdul Aziz Rimo na Abubakar Sharif Ahmed (almaarufu Makaburi), walikuwa wameteka baadhi ya misikiti ambapo walianza kuendesha mafunzo ya jihadi,” inasema ripoti hiyo.

Katika mwaka wa 1996 na 1997, mawaidha yaliyokuwa yanaendeshwa na Sheikh Rogo yakawa yanafuatiliwa kwa ukaribu na vijana waliokuwa na misimamo mikali akiwemo Saleh Ali Saleh Nabhan, Haruni Bamusa, Fumo Mohamed Fumo na Ahmed Salim Swedan.

Nabhan alidaiwa kuwa kiungo muhimu akiwa pamoja na Fazul Mohamed katika kupanga operesheni ya pili ya kundi la kigaidi la al-Qaeda nchini Kenya mnamo Novemba 28, 2002.

Ni kwa kupanga shambulizi hilo ambapo Sheikh Rogo alikamatwa na baadaye kuachiliwa huru mwaka 2005 na huo ukawa mwanzo wake kuibuka kama “mtetezi mkubwa wa masuala ya Kiislamu aliyetambulika Afrika Mashariki” jambo ambalo lilimwezesha kujenga ufuasi mkubwa na kuendesha propaganda za jihadi nchini.

Ni kupitia ushawishi wake ambapo aliingia na kukipa mafunzo kikundi cha Muslim Youth Centre (MYC) ambacho kilikuwa kimesajiliwa kama chama cha masuala ya jamii na kuwa na kamati yake katika msikiti wa Riyadha eneo la Pumwani jijini Nairobi.

Mwaka wa 2007 kikundi hicho kilikuwa kinaendesha mafunzo hayo ya itikadi kali kupitia kiongozi wake Ahmed Iman Ali ambaye alikuwa mwanafunzi wa Sheikh Rogo.

Baadaye kikundi hicho kilibadilisha jina na kujiita Al Hijra baada ya kuanza kumulikwa na maafisa wa usalama. Kikundi cha Al Hijra kilipata uongozi wa Sheikh Rogo na Sheikh Makaburi.

“Lakini kabla ya Al Hijra kuweza kuendeleza mafunzo yake vilivyo viongozi wengi waliokuwa wanajihusisha nacho wakiwemo Sheikh Aboud Rogo na Abubakar Sharrif (Makaburi) waliuawa,” inasema ripoti hiyo ya Bw Chome.

Hata hivyo, kabla ya kuuawa mnamo Agosti mwaka 2012 tayari Rogo alikuwa amesambaza mbawa zake hadi nchini Tanzania ambapo uchunguzi wa ripoti hiyo unasema kuwa wanachama wa chama cha Ansaar Muslim Youth Centre (AMYC) walipata mafunzo kwake.

Ilifichuliwa kuwa kikundi hicho cha AMYC kilikuwa kinaendesha mafunzo ya kushawishi vijana kujiunga na Al Shabaab na kufanyia mchango kundi hilo haramu.

Inaaminika kundi hilo lilikuwa linaendesha shughuli zake za kujipatia fedha kupitia kutumia kundi la wahuni wa Tanga kufanya biashara haramu ili kujiendeleza.

Nchini Msumbiji kundi hilo limedaiwa kutekeleza zaidi ya mashambulizi 120 ndani ya miezi mitatu pekee ya mwanzo wa mwaka 2020.