Habari MsetoSiasa

Ripoti yafichua pesa za CDF zinavyofujwa

May 12th, 2019 2 min read

Na SAMWEL OWINO

FEDHA za Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF) bado zinaendelea kutumiwa vibaya, ripoti ya ukaguzi wa matumizi ya fedha za umma iliyowasilishwa bungeni imeonyesha.

Ripoti hiyo ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw Edward Ouko, kuhusu matumizi ya pesa za NG-CDF katika mwaka uliokamilika Juni 30, 2018, inaelezea visa kadha vya kutokamilishwa kwa miradi licha ya kutengewa fedha za kutosha. Na katika baadhi ya maeneo bunge, miradi kadhaa haikuanza lakini pesa zilizotengewa ziliripotiwa kutumika.

Katika eneo bunge la Tetu, ripoti hiyo ilibaini kuwa Sh3 milioni zilizotengewa shule tatu, kila moja ikipokea Sh1 milioni, kwa ajili ya ukarabati wa madarasa na kukamilishwa kwa ujenzi wa afisi, hazikutumiwa vizuri.

Kwa mfano, Sh1 milioni zilitumwa kwa shule ya msingi ya Nyathithe kufadhili ukarabati wa madarasa manane lakini ukaguzi uliofanywa Januari 2018, ulibaini kuwa ukarabati ulifanywa kwa sehemu ya mbele pekee ya madarasa hayo.

Hakuna kazi yoyote iliyofanywa sehemu za nyuma ya madarasa husika kwani rangi haikupakwa katika paa na madirisha.

Hali ni hiyo hiyo katika Shule ya Msingi ya Kiwaithanji ambako licha ya Sh1 milioni kutengwa kwa ajili ya ukarabati wa madarasa manane, ni madarasa manne pekee yalikarabatiwa.

“Usimamizi wa shule haukutoa maelezo kuhusu ni kwa nini kazi haikukamilishwa. Kwa hivyo, thamani ya Sh1 milioni zilizotengewa ukarabati huo haingeweza kuthibitishwa,” Bw Ouko akasema.

Na katika eneo bunge la Soy ripoti hiyo inasema kuwa Sh800,000 zilitengewa ujenzi wa Shule ya Upili ya Moi’s Bridge. Hata hivyo, mradi huo hata haukutekelezwa.

Bw Ouko pia anatilia shaka matumizi ya Sh26 milioni zilizotengewa ufadhili wa miradi 39 katika eneo bunge hilo. Hii ni kwa sababu ukaguzi ulibaini kuwa miradi hiyo haikukamilishwa licha ya kamati ya usimamizi wa miradi kupokea pesa hizo.

Katika eneo bunge la Samburu Magharibi, Bw Ouko alitilia shaka matumizi ya Sh2.9 milioni zilizotengewa ujenzi wa maabara katika Shule ya Upili ya Wamba.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa zabuni ya mradi huo ilitolewa kinyume cha sheria.

Na wakaguzi walipofika shuleni humo Januari 2018, waligundua kuwa kazi ya kutengeneza mitambo ya kutoa maji chafu na kuunganisha nyaya za umeme haikuwa imekamilika.

Isitoshe, mwanakandarasi hakuwa eneo la kazi hivyo kuibua shaka ikiwa mradi huo utakamilishwa.

“Uhalali na thamani ya Sh2.6 milioni ambazo tayari zimetumiwa katika mradi huo kufikia Juni, 2018 hauwezi kuthibitishwa,” ikasema ripoti hiyo.

Katika eneo bunge la Kangema Sh5 milioni zilitumiwa katika ujenzi wa kituo kidogo cha polisi cha Kiawambogo . Hata hivyo, kituo hicho hakijaanza kufanya kazi.