Habari Mseto

Ripoti yaonyesha wabunge walitumia Sh25 milioni kujifurahisha Urusi

August 16th, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

Wabunge waliosafiri hadi Russia kushuhudia mashindano ya kandanda ya Kombe la Dunia  nchini Urusi wamewasilisha ripoti bungeni, wiki mbili baada ya spika Justin Muturi kuwataka kuelezea taifa kuhusiana na ziara hiyo, ambayo ilikashifiwa.

Jumla ya wabunge 17 walitumia kitita cha Sh25milioni kwa tiketi za ndege, vyakula na kupata makazi ili kusafiri ziara hiyo kutazama mechi za kombe la dunia, miezi miwili iliyopita.

Hii ni licha ya changamoto inazokumbana nazo Kenya ikijaribu kuongeza mapato ya pesa na kuinua miundomsingi katika sekta ya michezo, mbali na kuzongwa na madeni.

Mwenyekiti wa kamati ya michezo, utamaduni na utalii Victor Munyaka anaitaka serikali kujenga viwanja vinane vya hadhi nzuri katika maeneo yaliyokuwa mikoa mbeleni, ili taifa liweze kuchezesha michezo mikubwa.

Kamati hiyo aidha inataka viwanja vitano vikubwa vya kenya (CHAN) ambavyo ni Kasarani, Nyayo, Machakos, Kipchoge Keino na Kinoru kuinuliwa kufikia viwango vya FIFA.

Hii ni licha ya maombi ya kamati hiyo kwa wizara ya michezo kuwa ianzishe academia za kufunza michezo katika kila eneobunge ili kulea vipaji kutoka chini, na kufanikisha uundaji wa timu dhabiti.

“Timu za kandanda kenya kufikia sasa zinafaa kuwa na academia zao zilizoimarka ili kuinua viwango vya michezo nchini,” akasema Bw Munyaka.