Ripoti yaonyesha watu 43 ‘walipotezwa’ kipindi cha Januari hadi Novemba 2021

Ripoti yaonyesha watu 43 ‘walipotezwa’ kipindi cha Januari hadi Novemba 2021

Na KALUME KAZUNGU

KENYA imerekodi idadi ya juu zaidi ya watu waliopotea katika hali isiyoeleweka mwaka huu ikilinganishwa na miaka ya awali.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Haki Africa, jumla ya watu 43 walipotea katika hali tatanishi, wengine wakiwa mikononi mwa walinda usalama kati ya Januari na Novemba 2021.

Kwenye ripoti hiyo Ukanda wa Pwani bado unaongoza kote nchini kwa visa vya watu kupotezwa, ambapo ni visa 29 vilivyorekodiwa.

Kaunti ya Mombasa inaongoza kwa visa 17, ikifuatwa na Kwale ambayo ikona visa 9, Nairobi ikiwa na visa 7, Kajiado visa 4, Lamu ikiwa na 3 ilhali kaunti za Wajir, Nyeri na Kiambu zikiwa na kisa kimoja kwa kila moja.

Kwenye mahojiano na Taifa Jumapili, Mkurugenzi Mkuu wa Haki Afrika, Hussein Khalid, aliikashifu idara ya usalama nchini kwa kukiuka haki za binadamu waziwazi na kuendelea kuwapoteza raia kiholela.

Mkurugenzi wa Haki Africa, Hussein Khalid. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Khalid alitaja idadi ya watu 43 kuwa ya kutisha mno, hivyo akamtaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i kuingilia kati na kuhakikisha haki za wananchi hazikiukwi na walinda usalama.

“Kati ya Januari na Novemba 2021, tumerekodi idadi ya watu 43 ambao wamepotezwa nchini. Hii ndiyo idadi ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa katika kipindi cha mwaka mmoja hapa nchini. Tunaendeleza majadiliano na Waziri Matiang’i ili kuona kwamba familia zilizoathiriwa zinapata haki,” akasema Bw Khalid.

Ripoti hiyo inajiri wakati ambapo viongozi wa dini ya Kiislamu na wazee kisiwani Lamu mwishoni mwa wiki jana waliandaa maombi maalum ya kuwaombea waliopotezwa warudishwe salama.

Shughuli hiyo ilifanyika katika eneo la Mkunguni, chini ya mwavuli wa Bodi ya Viongozi wa Kidini (CICC).

Mwenyekiti wa CICC, Mohamed Abdulkadir pia aliiomba serikali kukoma kuwakandamiza wananchi kwakuwapoteza kiholela katikaharakati za kupigana na ugaidi nchini.

“Katiba ikowazi.Kwamba yeyote anayepatikana kukiuka sheria akamatwe nakuwasilishwa kortini badala ya kupotezwa. Hivi visa vya watu wetu klupotezwa ni ukandamizaji ambao pia unatia hofu jamii zetu. Lazima hali hii ikomeswe,” akasema Bw Abdulkadir.

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Miguu ya kuku chakula kitamu sana

Mganda avunja rekodi ya dunia mbio za kilomita 21...

T L