Makala

RIZIKI: Atumia elimu, ujuzi wake wa ukulima kuwaelimisha wanawake

October 24th, 2020 2 min read

Na MISHI GONGO

KATIKA eneo dogo la Vigujini eneobunge la Msambweni, Mwanasha Gaserego, 31, anatambulika kwa juhudi zake za kuwainua wanawake kiuchumi kutumia kilimo.

Yeye ni mkulima wa nyanya na sukumawiki.

Aliingilia kilimo ili kuituliza kiu yake ya kutaka kula mboga safi zisizo na kemikali.

Mwanasha alianza na kupanda tomato na sukumawiki sehemu ndogo tu ya shamba lake,kwa nia ya kujitosheleza hata hivyo mboga zake zilipopevuka majirani walianza kubisha hodi kutaka kununua bidhaa hizo ambazo ni adimu katika kijiji chao.

“Tuko na shida ya kupata mboga, tunalazimika kwenda mwendo mrefu kupata bidhaa hizi. Sikuwa na nia ya kuuza lakini nilipoona wateja wameogezeka niliamua kupanua sehemu niliyokuwa nimelima awali na kuongeza miche ya mboga,” akasema Mwanasha.

Pia alisema wahudumu wa vibanda huuza bidhaa hizo kwa gharama ya juu.

Mwanasha Gaserego akiwa katika shamba dogo la nyanya eneo la Vigujini, Msambweni, Kaunti ya Kwale. Picha/ Mishi Gongo

Mwanasha amesomea taaluma ya uwanahabari lakini baada ya kuona anapata kipato cha kutosha katika ukulima, alitupilia mbali juhudi za kusaka ajira afisini.

Alielezea kuwa alifanya taaluma hiyo ili kuwasaidia wanawake katika kijiji chake lakini amegundua kuwa anaweza kufanya hivyo bila kuajiriwa.

“Nia yangu ilikuwa kutumia vyombo vya habari kuwasilisha matatizo yanayowakumba wanawake katika jamii yetu lakini baadaye nilitambua kuwa matatizo mengi yanayowakumba wanawake nikutokana na wao kutokuwa huru kiuchumi, hivyo natumia elimu yangu ya ukulima kuwafundisha na wao,” akasema.

Mwanasha alieleza Akilimali kuwa siku yake huanza saa kumi na moja alfajiri.

“Baada ya kuswali, mimi huenda shambani kupalilia na kuvuna nyanya zilizoiva. Pia huangalia zile zilizo na maradhi na kuzikata,”akasema.

Alisema huuza ndoo ya lita 10 kwa Sh200 huku fungu la tomato nne akiuza kwa Sh10.

Wateja wake huwa wauza vibanda na wanaotaka kwa matumizi ya yumbani.

“Hapa sina bosi wa kunisimamia au kunikaripia. Mimi mwenyewe ndio najipanga vile ntaendesha biashara yangu. Nawalenga watu wa vitongojini ambao hawapati mboga safi kutokana na umbali wa miji yao na soko,” akasema.

Alisema kwa sasa ameweza kuwaajiri vijana wawili wa bodaboda ambao huzungusha nyanya na sukuma majumbani.

Anatangaza biashara yake mitandaoni na pia kwa mdomo ili kufikia wateja wake ambao hawana simu za kuwawezesha kuingia mitandaoni.

“Ninapokwenda katika shughuli mbalimbali za kijamii kama vile mazishi, sherehe za harusi, na mikutano, hubeba kiasi kidogo cha bidhaa zangu na kwenda kuonyesha wateja,” akasema.

Anasema ndoto yake ni kupanua ukulima wake aweze kuzalisha mboga mbalimbali katika shamba la ukubwa wa ekari 20 au zaidi.

Anawashauri vijana kuacha kusubiri kuajiriwa na badala yake kuingilia kilimo na kazi zingine za mikono kujipatia riziki.

“Vijana ndio wanatumiwa katika kutekeleza machafuko ya kisiasa, hii inatokea kwa sababu vijana wengi hawajajishuhulisha, tunapokuwa na kazi za kufanya hatutatumika kijinga tena,”akasema.

Alieleza kuwa kupitia biashara yake hupata Sh40,000 au zaidi kwa mwezi.

“Mwanzo nilikuwa sina ufahamu wa kutosha wa kupanda mboga; hivyo nilipata hasara ya mboga kushambuliwa na maradhi ya mimea na wadudu. Lakini kwa sasa nimesoma kupitia mitandao na kutoka kwa wataalamu wa kilimo na nimeweza kuwa gwiji katika ukulima,” akasema.

Alieleza kuwa hutumia mbolea ya kuku na mbuzi wake katika kuongeza rutba kwa mchanga kabla ya kupanda.

“Huenda katika Taasisi ya kilimo na utafiti, tawi la Kwale ili kupata mbegu bora,” akasema.

Alisema anatumia maji kutoka kwa ziwa lililo karibu nae kunyunyizia mimea yake.

“Ukulima haujanigharimu sana, niko na genereta ambayo natumia kupigia maji kutoka ziwani ili kunyunyizia mimea,”akaeleza Mwanasha.

Kupitia ukulima wa mboga ameweza kumsaidia mumewe kukimu majukumu ya nyuma yao.

Aliwahimiza wanawake kuacha kutegemea waume na kujitoa kimasomaso katika kutekeleza kilimo.