Makala

RIZIKI: Biashara ya mboga kienyeji yamfaa pakubwa

October 13th, 2020 3 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MIRIAM Nabakwe, mwenye uelewa wa biashara ya hoteli amekusudia kusaidia watu kuimarisha afya zao kwa kutoa jukwaa ambalo huleta vyakula vya jadi na mboga kienyeji hadi mlangoni pako.

Miriam alianzisha Kienyeji, sio tu kuhudumia idadi ya watu wanaokua wakipambana na magonjwa ya mtindo wa maisha kwa sababu ya lishe duni lakini pia kuwasaidia wale ambao hawajui wapi watapata mboga kienyeji na jinsi ya kuandaa.

Mama huyu wa watoto watatu pia hutumia jukwaa lake kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Aliacha kazi hii rasmi mnamo 2007 ili kuingia kwenye biashara ambayo alianza kama mshauri wa chakula na vinywaji.

Kwa kuwa mtaalam wa kahawa, Miriam ni jaji aliyethibitishwa na Kenya National Barista Championships na ana zaidi ya miaka kumi akifanya kazi ya ujaji na pia amehusika kikamilifu katika mafunzo ya wafanyakazi wanaohusika na chakula na vinywaji nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Katika Instagram tafuta @kienyejisstore.

“Biashara yangu inahusu kurudisha watu kwenye vyakula vilivyosahaulika. Ninatoa aina anuwai ya chakula cha protini na anuwai ya mchanganyiko tofauti zaidi ya kumi na tatu wa mboga za Kienyeji ambazo zimepikwa na kukaushwa, ”anasema

Anahisi kuwa biashara yake inampa urahisi mwanamke aliye na shughuli nyingi ofisini na watu wanaotamani kufurahiya chakula cha jadi lakini hawajui jinsi ya kuitayarisha, akijitahidi kuipa biashara yake mguso kutoka kwa historia yake ya vyakula na vinywaji.

Kutoka utotoni, Miriam alipenda kumuona babu na nyanya yake marehemu wakipika na hapo ndipo hamu yake ya kupika vyakula vya jadi iliongezeka.

“Babu yangu marehemu alikuwa mpishi wa Wamishonari na marehemu nyanyangu alikuwa muuzaji wa chakula. Kichocheo zaidi ni babangu ambaye amekuwa ni mzuri sana hadi leo hii. Chakula chake kila wakati ni cha kiasili,” anasema

Kupitia haya yote Miriam alijiapiza kuwa atafuata taaluma katika biashara ya chakula ambayo alianza hii katika shule ya upili kupitia masomo ya sayansi ya nyumbani.

Miriam Nabakwe ambaye huuza mboga kienyeji akiwa katika picha ya pamoja na wenzake. Picha/ Margaret Maina

“Niliishia kufanya kazi katika hoteli kadhaa nikiwa na majukumu muhimu katika menejimenti na wakati wote wa safari yangu ya kuajiriwa, nilikuwa nikifanya biashara ya chakula pembeni. Nilijua kuwa siku moja nitakua na chapa yangu ya chakula,” anasema

Anaongeza: Nilianzisha Kienyeji mwaka 2014 baada ya kujaribu biashara zingine nyingi ambazo hazikuwa sawa kwangu na nilihitaji kufanya kitu tofauti. Mama yangu alinitumia gunia la mboga asili kutoka kijijini na wateja wangu wa kwanza walikuwa marafiki wangu wa karibu.”

Kwa miaka yote hiyo, Miriam aliendelea kukua na kukuza maoni ya kupendeza kuhusu vyakula. Anakubali kuwa anaweka vyakula hivyo asili na halisi.

“Ubora wangu bora ni akili yangu ya ubunifu. Hii imeniwezesha kupata mchanganyiko wa aina zaidi ya kumi na tatu ya mchanganyiko wa mboga za Kienyeji na vitu vya protini, ”

Pia ana mboga zilizokaushwa juani kutoka kwa kijiji chake katika Kaunti ya Bunyore Vihiga na kupelekwa Nairobi kwa basi kabla ya kupakiwa na kuuzwa.

“Wateja wangu wengi ni wazee, wale ambao wanakosa mboga za kienyeji ambazo wanajua wanaweza kupata tu labda katika vijiji vyao na sasa wanaweza kuzipata mjini, pia wale wanaopenda mboga hizi lakini hawajui jinsi ya kuandaa,” akasema.

Miriam Nabakwe (kulia) ambaye huuza mboga kienyeji. Picha/ Margaret Maina

Anaongeza kuwa kuwasikiliza wateja wake na mahitaji yao, hasa ikiwa wanahitaji mboga maalum ndio ambayo imechangia sana ukuaji wake.

“Biashara yangu ni ya nyumbani. Ninatumia majukwaa yangu ya kijamii kujiuza. Ninatamani siku moja kuwa na eneo halisi lakini niliamua kuwa ukosefu wa rasilimali hazitakuwa kikomo changu,” anasema

Miriam ameazimia kuendelea kujiendeleza kutoka nyumbani kwake wakati anafanya kazi kupitia ukuaji wake hadi kupata eneo.

Uzuri kuhusu biashara hii ni kuweza kutoa ajira kwa watu. Ninafanya kazi na wanawake ambao ni wazazi wasio na waume – single mothers – na wajane. Hii inatimiza sana kuwaona wakiweza kutunza familia zao kupitia biashara hii.

Anasema kuwa bado anahisi kama bado hafanyi kazi kwa uwezo wake wote,

“Ninayo mipango mizuri ya maendeleo na niliapa mwenyewe kuzingatia na kuhakikisha kuwa nitaona maono yangu siku moja yatatimia.”