Makala

RIZIKI: Corona imebadilisha maisha yangu kuwa ya kutegemea

April 28th, 2020 2 min read

Corona imebadilisha maisha yangu kuwa ya kutegemea ilhali yalikuwa ya kusaidia

Na SAMMY WAWERU

MACHI 2020 Rais Uhuru Kenyatta aliagiza shule zote za msingi, upili na taasisi za juu za elimu kufungwa mara moja kwa muda usiojulikana kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona nchini.

Rais alichukua hatua hiyo ili kusaidia kuzuia maambukizi ya virusi hivyo hatari vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Jecinta Karimi ni mmoja wa wazazi. Ana watoto wawili, mwenye umri wa miaka minane aliye gredi ya tatu na mwingine umri wa miaka mitatu, ambaye yuko chekechea, wote wakiwa na bahati kuwa chini ya mfumo mpya wa masomo nchini.

Hata ingawa likizo hiyo ya mapema na lazima hakuwa amejiandaa, anasema hakuwa na budi ila kubadilisha ratiba yake. Kwa kawaida, mama huyo ambaye ni mkazi wa Nairobi, likizo ya mwezi Aprili, Agosti na Disemba, zinapobisha hodi hutafuta kibarua wa muda kumtunzia wanawe, ili aweze kuendesha biashara yake.

“Mara hii singemudu kwa sababu ya athari za corona. Nimelazimika kukaa na watoto wangu,” Jecinta anadokeza. Mwezi mmoja wanafunzi wakiwa nyumbani umekamilika, na Waziri wa Elimu Prof George Magoha alitangaza nyongeza ya likizo ya mwezi mmoja zaidi, shule zikitarajiwa kufunguliwa Juni 2020 kulingana na hali itakavyokuwa.

Jecinta ana duka la kuuza bidhaa za urembo, kama vile nywele, mafuta na manukato, ambapo pia hufanya shughuli za ususi, eneo la Roysambu, Nairobi.

Tangu kisa cha kwanza cha maambukizi ya Covid-19 kuripotiwa nchini, biashara nyingi zilianza kudorora na kukadiria hasara.

Jecinta anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba biashara yake haikuepuka mjeledi huo.

“Mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili nililazimika kuifunga. Idadi ya wateja ilishuka mara moja, siku nyingi zingepita bila kufanya mauzo yoyote,” anafichua, kiwango cha wateja kupungua kikichangiwa na hofu ya maambukizi ya corona.

Isitoshe, kodi ya chumba cha biashara anasubiriwa kulipa mwishoni mwa mwezi.

Mama huyo anasema kwa sasa anategemea ‘mkono mmoja’ kukidhi familia riziki, mume wake, na ambaye anasema anakofanya kazi mambo yanaonekana si shwari.

“Tulikuwa tukisaidiana kukimu familia. Anakofanya kazi mume wangu wamepata notisi ya kupunguzwa mshahara, maisha yanazidi kuwa magumu kila uchao,” Jecinta analia, akiongeza kusema kwamba tayari ajenti wa ploti wanayoishi ameanza kuwabishia mlango akiwakumbusha kodi inapasa kulipwa.

“Ni watoto tutalisha au ni kodi tutalipa?” anashangaa.

Uchumi unaendelea kuyumbishwa na janga la corona, ambalo kwa sasa linatikisa ulimwengu mzima. Si maambukizi mapya kuripotiwa kila siku, si vifo na watu kuwekwa kwenye karantini, matukio hayo yote ukiyajumuisha yanakuna watu akili na vichwa.

Masaibu ya Jecinta Karimi kufunga duka lake kwa sababu ya athari za corona, yanathibitisha biashara, kampuni na mashirika yalivyoathirika, huku watu wakipoteza kazi, kupewa likizo ya lazima na hata kupunguzwa mishahara.

Mama huyo anasimulia kwamba maisha yamekuwa “kusalia kwenye nyumba na wanawe”. Amri ya Rais Kenyatta ya kutoingia na kutotoka kaunti ya Nairobi na viunga vyake, imemzuia kuelekea mashambani, eneo la Embu.

“Mashambani maisha ni rahisi kwa kuwa chakula ni kingi, nitaweza kulima na sitahangaika kulisha watoto wangu, ila kafyu hainiruhusu kuenda humo. Pakiti ya kilo mbili unga wa mahindi, tunaila kwa siku mbili pekee, hali isipoimarika huenda tukaanza kulala njaa,” Jecinta anaelezea.

Bi Jecinta Karimi. Asimulia mazito anayopitia baada ya kufunga biashara yake kufuatia athari za corona. Picha/ Sammy Waweru

Licha ya kuwa serikali imeibuka na mikakati ya kutoa chakula cha misaada kwa Wakenya, inalenga wakazi wa mitaa ya mabanda.

Kaunti ya Nairobi na Mombasa, zimetajwa kuongoza katika maambukizi ya Covid – 19, na ni suala linalomtia wasiwasi mama huyo. Ana imani Kenya itashinda vita dhidi ya corona, kila siku akipiga dua kwa Mwenyezi Mungu kuondolea ulimwengu janga hili linalotesa.

Hata hivyo, anasema ushindi huo utajiri Wakenya wakifuata taratibu na sheria zilizotolewa na wizara ya afya kuzuia maambukizi zaidi.

“Tukishirikiana kwa kufuata taratibu na sheria zilizotolewa na serikali tutashinda janga hili turejelee maisha yetu ya kawaida, la sivyo maambukizi yataendelea kushuhudiwa,” ahimiza mama huyo.