RIZIKI: Funzo la Covid-19 katika suala la ajira

RIZIKI: Funzo la Covid-19 katika suala la ajira

Na SAMMY WAWERU

MONICA Mwangi alikuwa amepiga hatua nyingi mbele kimaendeleo katika sekta ya uuzaji wa mashamba na ujenzi wa nyumba aliyokuwa ameajiriwa.

Licha ya kuwa amesomea kozi inayohusiana na masuala ya kibinadamu, Monica anasema uuzaji wa ploti na mashamba ni kazi yenye mapato makubwa.

Mlipuko wa janga la Covid-19 nchini mnamo Machi 2020 hata hivyo ulikatiza jitihada za mama huyu. “Uuzaji wa ploti na mashamba unahitaji mmoja kusafiri kukutana na wateja, sheria na mikakati iliyowekwa na serikali kusaidia kuzuia maenezi ya virusi vya corona, hasa zuio la usafiri na uchukuzi, ziliathiri utendakazi,” Monica anasema.

Ni janga la kimataifa ambalo lilijiri na mafunzo mengi. Kuanzia sekta ya utalii, biashara, uchukuzi na usafiri, afya, kilimo…zote ziliathirika.

Mamia na maelfu ya watu walipoteza nafasi za ajira.

Licha ya Monica ambaye ni mama wa watoto watatu kuwa katika sekta ya kilimo, ila alikuwa akikiendeleza kwa njia ya simu, Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa corona, alilazimika kukiingilia kikamilifu.

Hukuza mseto wa mimea, kuanzia brokoli, spinachi, vitunguu, bitiruti na matango.

Ni janga analosema limejiri na funzo, hasa kwa wanaotegemea ajira za ofisini.

Monica Mwangi alikuwa katika sekta ya uuzaji ploti na mashamba, ila janga la Covid-19 liliiathiri kwa kiasi kikubwa. Aliingilia shughuli za kilimo na ambazo zimemuwezesha kukidhi familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi. Picha/ Sammy Waweru

“Kilimo kiliniokoa kukidhi familia yangu riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi,” anasema.

Wengi wa walioathirika kufuatia mkurupuko wa Covid-19, waliingilia shughuli za kilimo na ufugaji.

Huku baadhi wakidunisha kilimo, wakikitaja kama gange inayopaswa kufanywa na wazee na waliostaafu, kwa Monica ni dhahabu.

“Licha ya kwamba biashara ya uuzaji wa ploti na mashamba inaanza kurejea, sitaacha kilimo. Huenda siku za usoni kikawa chaguo langu la kwanza la kazi, gange zingine ziwe za ziada,” anaelezea, akidokeza kuwa anaendelea kutafiti namna ya kuunda mvinyo na divei itokanayo na bitiruti.

“Changamoto zinazokumba wakulima ni kuwepo kwa mawakala, ambao wamevamia soko la mazao ya kilimo na kuharibu bei,” anasema mkulima huyo, akihimiza wakulima kukumbatia suala la uongezaji mazao thamani.

Pauline Kinja, ni mmoja wa wafanyabiasbara wa mazao mabichi ya kilimo. Aliingilia biashara hiyo baada ya kazi yake ya upishi, japo ya kujiajiri, kusambaratishwa na virusi vya corona.

“Nilipogundua bidhaa nyingi za kilimo, hususan mbichi kama vile matunda yanaharibika upesi nilianza kuyaongeza thamani kwa kutengeneza juisi,” Pauline anaelezea, akidokeza kwamba pia huunda maziwa ya mtindi (yoghurt) yenye viungo vya matunda.

Janga la Covid-19 limepevusha wengi mawazo, likiwatahadharisha kazi za kuajiriwa ni za muda tu.

“Ajira yenye uhakika wa usalama wayo ni unayomiliki. Ni muhimu watu watathmini mawazo yao, wajiandae kwa kuwa na shughuli za ziada kuwaingizia mapato,” anashauri Jack Kamau, mtaalamu wa masuala ya fedha na kiuchumi.

Huku wengi wa waliopoteza ajira kipindi cha corona wakisaka njia mbadala kujiendeleza kimaisha, Kamau anasema janga linapotukia mwajiri pia hasazwi na anapokadiria hasara njia mojawapo anayoipa kipau mbele kupunguza gharama ya matumizi ni kwa kuchuja idadi ya wafanyakazi.

“Baadhi ya mashirika na kampuni, tumeona yakipunguza mishahara. Wewe kama mfanyakazi unapaswa kujiandaa kwa lolote, kwa njia ya kujipanga,” anasisitiza.

Kimsingi, janga la corona linapaswa kuwa funzo kwa kila mmoja, katika maandalizi ya jukwaa mbadala kujiendeleza kimaisha.

  • Tags

You can share this post!

Majeshi pinzani ya Somalia yakabana

Bobi Wine akerwa na kimya cha viongozi wa bara Afrika