Makala

RIZIKI: Habagui kazi licha ya kuwa mhitimu

March 5th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MWANADADA huyu ni mhitimu wa mwaka 2012 lakini kufikia sasa analazimika kufanya kazi za juakali kwa sababu hajawahi kupata ajira ya afisini.

KWA mujibu wa takwimu za sensa ya 2019 iliyotolewa na KNBS siku kadha zilizopita, vijana 5,341,182 kati ya 13,777,600 hapa nchini hawana ajira.

KNBS ilieleza vijana walio na umri kati ya miaka 18 – 34, ndio wameathirika kwa kiasi kikuu, ikilinganishwa na walio na zaidi ya miaka 35.

Hayo yanaashiria ugumu wanaopitia vijana, katika mchakato mzima kutafuta kazi chini ya mazingira magumu ya uchumi wa sasa na ambao unaendelea kudorora kila uchao.

Vijana wanapotajwa kuathirika, hilo linagusa kila dira ya taifa, kuanzia mpaka wa Malaba hadi Namanga, kuelekea Pwani ya Kenya, na kurejea hadi Moyale. Huo ukiwa mfano tu.

Isitoshe, vijana wanaendelea kufuzu kwa vyeti mbalimbali vya masomo kutoka taasisi za juu za elimu, kila mwaka. Ukosefu wa ajira miongoni mwao ni jambo bayana kuwa donda ndugu, hasa hapa nchini Kenya.

Hilo linapozungumziwa, Joyce Wambui anajumuishwa kwenye listi ya mamilioni ya vijana hao. Ni msomi wa masuala ya biashara, ambapo miaka saba iliyopita alifuzu kwa shahada kutoka chuo kikuu kimoja hapa nchini.

“Mwaka 2012 nilivalia mavazi rasmi na taji la kufuzu shahada inayohusisha masuala ya biashara,” Wambui anaeleza.

Alijiunga na vijana wenza kusaka kazi, angaa kusukuma gurudumu la maisha.

Ni safari anayosema imesheheni milima na mabonde, bila kusahau mazingira mengine aliyokuta miamba isiyotikisika.

“Nikitoa nakala za wasifu nilizoandaa pamoja na barua za kuomba kazi na vyeti, utashangaa,” anasimulia.

Shughuli hizo alizivalia njuga kwa muda wa miaka mitano mfululizo, akikariri kuwa amezuru karibu kila kona ya jiji la Nairobi katika kile anataja kama kutafuta mashirika na kampuni kuomba nafasi ya kazi.

Wachache waliompa mwaliko wa kupigwa msasa, anasema waliahidi kumueleza ikiwa amefua dafu ahadi ambazo anasubiri kufikia leo.

“Kampuni mbili pekee ndizo zilinipa nafasi ya kupata mafunzo, bila mshahara. Zilikuwa zikigharamia nauli, na baada ya miezi sita hadi mwaka mmoja, kila moja ilidai nafasi ya kazi ikitokea ningeitwa,” adokeza.

Wambui 31, anasema alichoshwa na mahangaiko hayo, akaamua kuingilia vibarua vya juakali. Licha ya kuwa na shahada, mwanadada huyo habagui kazi, iwe ya dobi, mijengo au hata huduma za ziada kwenye mikahawa mitaani, bora iwe ni halali.

Wakati wa mahojiano tulikutana na kijana huyo ambaye ni mama wa mtoto mmoja, miaka minne, eneo la Mwihoko, Kaunti ya Kiambu, kwenye mkahawa mmoja, ambapo anafanya huduma za ziada kuwahudumia wateja.

“Huingia saa moja na kufikia saa tisa saa kumi hivi, hukunja jamvi ili kufanya kibarua kingine,” akasema.

Alifichua kuwa majira ya jioni, huchuuza kahawa na mahamri.

“Maisha sharti yasonge mbele, familia ipate riziki na kujiendeleza kimapato,” anasema.

Kulingana na Wambui, maazimio yake ni kuona ameweza kujiajiri kwa kuweka biashara. ”Awali nilidhani kazi za ofisi ndizo zina mapato pekee, nisijue sekta ya juakali ndiyo imeshikilia uchumi,” anasema, akiongeza kuwa lengo lake ni kuanzisha mkahawa.

“Haijalishi hadhi ya mkahawa, ninalenga wenye mapato madogo.”

Sekta ya juakali na pia SMEs hukadiriwa kuchangia zaidi ya asilimia 75 ya nguvukazi nchini, na kulingana na Anderson Kimathi, mtaalamu wa masuala ya biashara na uchumi anasema serikali inapaswa kukaza kamba jitihada zake kupiga jeki sekta hiyo.

“Wengi wa wateja wetu wanatoka sekta ya juakali. Ni muhimu iangaliwe kwa njia ya kipekee. Mazingira yao ya biashara yaimarishwe,” anahimiza Kimathi ambaye ni meneja wa chama cha ushirika cha Southern Star tawi la Githurai.