Makala

RIZIKI: Hiki kinaweza kuyumba Mungu akakujalia kile

March 8th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

BI Annitah Njeru ni mtulivu na mwenye tabasamu unapotangamana na kushiriki mazungumzo naye.

Ni mzaliwa wa Kerugoya, Kaunti ya Kirinyaga, na ni huko ndiko anakofanya kazi katika afisi ya usajili na utoaji wa vitambulisho, kazi anayosema aliipata kiurahisi, lakini baada ya kuhangaika kwa muda mrefu.

Mwanadada Annitah na ambaye ni mama wa mtoto mmoja – mwenye umri wa miaka minane – anasimulia kwamba pindi tu baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, 2006, alijiunga na taasisi moja ya mafunzo ya usektretari- uhazili – Nyeri, ambapo alisoma kwa muda wa miaka miwili.

Anasema hata baada ya kufuzu, haikuwa rahisi kupata kazi na hakuwa na budi ila kufanya vibarua vya hapa na pale, angaa kuzimbua riziki.

Vibarua vya kuchuuza nguo na hata kulima, vyote alivifanya, ili kuona analisukuma gurudumu la maisha.

Ni katika pilkapilka hizo, ambapo alikutana na mwanamume mmoja, anayesema kwamba walichumbiana kwa miezi kadhaa, kilele kikawa kuwa mume na mke.

“Nilitamani kuanzisha familia, na kulingana na ahadi zake alionekana mkomavu. Baada ya kujuzana kwa wazazi wa pande zote mbili, tulipata baraka zao tukaanzisha boma,” anaeleza.

Matunda ya ndoa ni kujaaliwa mtoto au watoto, na miaka miwili baadaye, walipata mtoto wa kike.

Annitah, 32, hata hivyo anasema mume wake alitamani kupata mtoto wa kiume, na hapo ndipo mgogoro kati yake na mume ulianza.

Kilichoanza kama mzaha mzee, akimaanisha mume wake, kufika akiwa ameshiba kilitunga usaha.

Kulingana na simulizi ya mama huyo, mavyaa na mashemeji zake walichangia kuchochea mumewe amuache, na hatimaye alimpa talaka. Binti wa wenyewe hakuwa na budi ila kurejea kwao, bila mbele wala nyuma.

Elizabeth Karungari, muuguzi mstaafu na mshauri wa masuala ya ndoa na familia, anasema changamoto za aina hiyo zinashuhudiwa mara kwa mara katika jamii, hasa ikiwa mume hataelewa kuwa huchangia kwa kiasi kikuu katika jinsia, wakati wa kujamiiana kutafuta mtoto.

“Mbegu za kiume kwa kushirikiana na za kike ndizo huamua jinsia ya mtoto. Si kisa kimoja au viwili nimetatua mume akilaumu mke kuzaa jinsia ambayo yeye (mume) hakutarajia,” Elizabeth anasema, pia akiongeza kuwa mume anapohusisha wanafamilia katika ndoa yake haswa masuala yanayoshirikisha mume na mke, uwekezano wa ndoa hiyo kudumu ni wa chini mno.

Kwa mujibu wa simulizi ya Annitah, mashemeji zake hawakutaka kumuona, kiasi cha kutafutia mumewe mke mwingine, tukio ambalo walilifanya hadharani.

“Wazazi wangu walinipokea. Walinisaidia kwa hali na mali,” anasema.

Mwaka mmoja baadaye, Annitah anasema aliingia kwenye ndoa nyingine. Hiyo nayo, hata ingawa hakujaaliwa kupata mtoto, ilijaa dhuluma na mateso, kwa anachotaja “mzee alikuwa mlevi kupindukia”. Aliamua kuondoka, miaka miwili baadaye, akihisi ameshiba vitushi na sarakasi za ndoa.

Mwanadada huyo anaiambia Taifa Leo kwamba 2015 alikumbuka ana vyeti vya usekretari, akaanza oparesheni ya kusaka kazi tena.

Japo halikuwa zoezi rahisi, anasema haikuchukua muda mrefu kupata nafasi ya kazi ya ukarani katika afisi ya usajili na utoaji wa vitambulisho Kerugoya, ambako anafanya kufikia sasa.

“Kila siku nilikuwa namsihi Mungu, asininyime ndoa na kazi. Alinijaalia kazi,” anadokeza, baraka anazosema zilimjia wakati alizihitaji kwa hali na mali, ikizingatiwa kuwa alikuwa na majukumu ya uzazi, kulea bintiye.

Kando na kazi ya kuajiriwa, Annitah ni mkulima eneo la Kirinyaga na pia anasema wikendi na wakati wa likizo hufanya uchuuzi wa nguo. “Huziendea jijini Nairobi, ninazichuuja muda wangu wa ziada kujipa pato la ziada,” anafafanua, akisema anapania kufungua duka, aajiri mfanyakazi atakayemsaidia kujiimarisha.

Isitoshe, mbali na baraka za kazi na biashara, anafichua kuwa amejaaliwa mchumba ambaye hivi karibuni kengele za harusi ‘zitapigwa’, kualika watu kusherehekea wakifunga pingu za maisha na kuonjesha waalikwa keki.