Makala

RIZIKI: Kijana ataja mambo muhimu ya kuzingatia katika biashara

January 24th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

ENEO la Progressive lililoko mtaani Githurai, ni lenye shughuli nyingi za uchukuzi, biashara na uwekezaji wa majumba na vyumba vya wapangaji kuishi kwa kulipia kodi.

Ni katika eneo lilo hilo tunakutana na kijana Samuel Kariuki, ambaye ni mmoja wa waliojituma katika sekta ya biashara.

Anamiliki duka la uuzaji wa bidhaa za kula, kama vile biskuti, mahamri, vinywaji aina ya soda na maziwa. Duka la Kariuki pia lina balbu, nyaya nyepesi za kusambaza nguvu za umeme miongoni mwa bidhaa zingine nyingi.

Aliingilia biashara hiyo ipatayo miaka mitatu iliyopita, baada kuhudumu kwa mkokoteni.

Aghalabu, vijana wengi wanapofanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, hasa wenye uwezo kifedha hujiendeleza kimasomo katika chuo kikuu au taasisi ya elimu ya juu.

Kariuki, 23, anasema miaka mitano iliyopita, baada ya kufanya KCSE, hakuweza kujiendeleza kimasomo kwa kile anataja kama ukosefu wa karo. Akiwa mzaliwa wa pili katika familia ya watoto watano, anasema wavyele wake walimudu kumsomesha hadi shule ya upili pekee.

“Walijaribu kadri wawezavyo nihitimu shule ya upili. Niliwapa fursa angaa wasomeshe wazawa wangu wafikie nilipo,” aelezea.

Kariuki, mzaliwa wa Kaunti ya Murang’a, alienda Nairobi kutafuta kazi aweze kusukuma gurudumu la maisha.

Anasimulia kwamba 2015, kazi iliyomlaki ni ya uchuuzaji wa maji kwa mkokoteni na kubebea watu mizigo.

“Kwa siku nilikuwa nalipwa mshahara wa Sh300,” afichua.

Aliye na hamu ya kupanda juu hukesha, matamanio ya Kariuki yalikuwa kumiliki mkokotoni wake binafsi na 2016 alifanikiwa kununua. “Niliununua Sh10,000 nikawa nimejiajiri,” asema.

Ni katika harakati za kukusanya haba na haba, ambazo hujaza kibaba, Kariuki alikutana na mmiliki wa duka moja Githurai, na duka lake lilikuwa lenye shughuli nyingi.

Barobaro huyo anasimulia kwamba kwa muda wa karibu saa mbili waliozama kwenye humzo, alikuwa amehudumia zaidi ya wateja ishirini. “Mmiliki alinifichulia muda huo alikuwa ameunda faida isiyopungua Sh200, kupitia uuzaji wa bidhaa ndogo ndogo za kula na za nguvu za umeme,” Kariuki anasema.

Upesi upesi, akakokotoa hesabu, “ina maana siku nzima (kwa siku) hakosi kutia kapuni faida isiyopungua Sh1,000”.

Ni wazo lililomkuna kichwa, akawaza na kuwazua akilinganisha mapato ya mfanyabiashara huyo na yake ambayo anasema yalikuwa kadri ya Sh500 kwa siku, yakienda juu sana siku bora angekwachua Sh700.

Isitoshe, huduma alizotoa ni sawa na mchezo wa pata potea, ambapo angepata vibarua au la. Kazi iliyompa afueni ni uuzaji wa maji, lakini haikutabirika.

Alifanya Hesabu, moja kuongeza moja ni mbili, ila si moja. Alienda akitafakari, hata siku zilizofuata wakati akiwa katika gange yake.

Hatimaye, alipata jawabu, “nitajaribu kuwekeza katika bidhaa rejareja za kula, hata walio katika biashara hiyo wanajiendeleza kimaisha, na baadhi yao wamefanya makuu na waliamua liwe liwalo, faida au hasara, gurudumu la maisha sharti lisukumwe”.

Katika jitihada zake, Kariuki alianza kuweka akiba kile kiduchu alichopata na kufikia mwishoni mwa 2016 alikuwa ameweka kibindoni Sh30,000.

“Nilitafuta duka, nikaanza kwa bidhaa kidogo,” aeleza.

Rafikiye, mmiliki wa duka lililostawi alimpatanisha na wauzaji wa kijumla. Hata ingawa matunda hakuanza kuyapokea mara moja, anasema mwaka mmoja baadaye alianza kuyaonja.

Jack Kamau, mtaalamu wa masuala ya uchumi na fedha anasema katika biashara yoyote ile, inahitaji muda kuanza kupata faida. “Faida ni mapato baada ya kuondoa gharama ya matumizi, na baada ya kurejesha mtaji, inaswa kugharamia bidhaa za kuiendeleza, kodi na hata leba. Hayo yote yanahitaji muda,” asema.

Kulingana na mdau huyo, kila biashara iwe ndogo au kubwa, kwa mfano; uuzaji wa mayai au gari, lazima rekodi iwepo.

Anasema, kila bidhaa inayonunuliwa inapaswa kurekodiwa – na pia inapouzwa – ili kutathmini ikiwa imeleta faida.

Miaka mitatu baadaye, Kariuki anasema anaona kazi yake imestawi na kunoga.

“Hata ingawa sijaalika mkaguzi wa hesabu kujua thamani ya hii biashara, kwa kutazama kwa macho inaonekana imekua,” akaambia ‘Taifa Leo’ wakati wa mahojiano.

Aidha, alifichua kwamba ameajiri kijana mmoja, ambapo biashara hiyo huhudumu zaidi ya saa kumi na mbili kwa siku.

Kijana Samuel Kariuki, alianza kama mhudumu wa mkokoteni, sasa ni mmiliki wa duka la bidhaa ambapo anauza vyakula na bidhaa nyinginezo.