Makala

RIZIKI: Kozi za mikono na kiufundi ni muhimu kukabili tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana

October 9th, 2020 2 min read

Na SAMM WAWERU

TAKRIBAN asilimia 75 ya nguvukazi nchini imewakilishwa na sekta ya juakali na ile ya biashara ndogondogo na za kadri, SMEs.

Ni sekta ambazo zinahusisha kazi ya mikono na kozi za kiufundi, kupitia utengenezaji wa vifaa na bidhaa tofauti tunazozitumia mara kwa mara.

Chini ya utawala wa serikali ya Jubilee, inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto taasisi zinazotoa mafunzo ya kiufundi ndizo Tvet zimeonekana kuimarishwa.

Awali, kabla ya tofauti za kisiasa kuonekana kuibuka kati ya Rais Kenyatta na Naibu wake, Dkt Ruto kwenye ziara mbalimbali za kikazi nchini alikuwa katika mstari wa mbele kupigia upatu ustawishaji wa taasisi hizo, akisema “ili kupata mwangaza nyumbani tunahitaji mafundi wa stima, kuvalia nadhifu tunahitaji mafundi wa nguo, kurembesha kichwa wasusi na vinyozi ndio wataalamu, mamekanika, ujenzi wa nyumba…miongoni mwa kazi nyinginezo za kifundi”.

Hata ingawa hatua ya Naibu wa Rais kusambazia vijana na kina mama vifaa vya kiufundi, kama vile toroli, mikokoteni, vifaa vya kusuka na pia kunyoa, kati ya vinginevyo inakosolewa na wapinzani wake, mpango huo ukiwa na mikakati bora na faafu, kwa kiasi fulani ni njia mojawapo kuimarisha sekta ya Juakali.

Rebecca Wanjiku ambaye ni msusi na mshonaji wa nguo, anasema ikiwa kuna jambo asilojutia maishani ni kusomea kozi za mikono.

Mwaka wa 2006 baada ya kulazimika kutia kikomo ari yake kuwa daktari ama mwanahabari, Wanjiku alijiunga na chuo kimoja kinachotoa mafunzo ya kushona nguo.

Baadaye, mwanadada huyo ambaye ni mama wa watoto wawili, alijifunza ususi na shughuli zingine kurembesha wanawake.

“Sijutii kamwe kufanya kozi za mikono, ni sanaa inayolipa vizuri,” anaeleza mjasirimali huyo ambaye amewekeza katika biashara ya ususi na nguo.

Anahimiza: “Serikali ikipiga jeki taasisi za kifundi na kuzitilia maanani, taifa litakuwa na vipaji wa kutosha jambo ambalo litaimarisha sekta ya Juakali na SMEs.”

Rebecca Wanjiku ni msusi, mrembeshaji na mshonaji wa nguo. Picha/ Sammy Waweru

Vipaji wapo, ila uhamasishaji kuwaimarisha unahitajika. Operesheni hiyo inapaswa kuanza wanakonolewa bongo, yaani taasisi zinazotoa mafunzo, ili watakapofuzu wawe na msingi bora kujiendeleza kimaisha.

Edward Gikaria ni mchoraji hodari, sanaa anayoisifia kumuwezesha kujiendeleza kimaisha. “Niliacha ualimu kufuata talanta yangu katika uchoraji. Nimesomea ualimu, ila ninafanya vyema katika sanaa, hebu jiulize iwapo ningesomea uchoraji ningekuwa wapi?” Gikaria anahoji, akihimiza vijana wenzake kukumbatia kozi za mikono.

Kwa nujibu wa mukhtadha wa vijana hao, ni wazi kozi za mikono na kiufundi zina mapato ya kuridhisha na ni muhimu serikali kukaza kamba jitihada zake kuimarisha taasisi zinatoa mafunzo hayo.

Ikizingatiwa kuwa kila mwaka maelfu ya vijana hufuzu kwa vyeti vya taaluma mbalimbali, waliosomea kozi za kiufundi wana nafasi murwa kujiajiri.

Mbali na kuwahami kwa mafunzo hayo, ni muhimu pia wapigwe jeki kifedha ili wajiunge na sekta ya Juakali na ambayo imekuwa na mchango mkuu katika kufadhili serikali, kupitia ushuru.

Kwa kufanya hivyo, suala la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana litaangaziwa na kutatuliwa.