Makala

RIZIKI: Licha ya kushinikizwa kusomea umekanika amefanikisha nyingi za ndoto zake katika biashara

December 31st, 2019 3 min read

Na SAMMY WAWERU

MTAA wa Mumbi ulioko eneobunge la Ruiru katika Kaunti ya Kiambu ni wenye shughuli mbalimbali, kuanzia biashara, uchukuzi kwa njia ya vijigari vya magurudumu matatu aina ya tuktuk na bodaboda.

Pia, kuna mabwanyenye waliowekeza kwenye majumba ya kupangisha, hususan ya makazi na kuendeshea biashara.

Ni katika mtaa huohuo Bw Antony Mwangi amewekeza kwenye biashara ya malimali. Huuza bidhaa za kula, za stima kama vile nyaya na balbu.

Duka la Mwangi mwenye umri wa miaka 32, pia lina mishipi, kofia, vitambaa vya kupiga chafya na kuchemua, miongoni mwa bidhaa zingine nyingi.

Aliingilia biashara hiyo miaka mitatu iliyopita, hatua anayosema ilimgharimu mtaji wa takribani Sh50,000.

“Nilikuwa na kontena, fedha hizo nilizitumia kununua bidhaa kutangulia kazi,” asema Antony.

Hata hivyo, mfanyabiashara huyo kabla afikie alipo sasa anasema maisha yake yamekuwa yenye changamoto tele. Baada ya kuhitimu kidato cha nne 2008, anasema wazazi wake walimshinikiza kusomea kazi ya umekanika na ni hatua ambayo haikumridhisha kamwe.

“Nilifanya kozi hiyo mradi tu niwaridhishe wazazi,” aelezea Bw Antony ambaye ni baba ya watoto wawili.

Hata ingawa suala la wazazi kuchagulia watoto wao taaluma linakosolewa na wasomi, barobaro huyo anasema hakuwa na budi ila kuheshimu msimamo wao.

Miezi kadhaa baadaye, alijiunga na mamekanika wenza, baada ya kuhitimu. Furaha yake haikuwa humo, na anasema aliishia kuwa utingo wa magari yanayohudumu kati ya jiji la Nairobi na mtaa wa Kayole.

“Wazazi hukosea kuchagulia watoto wao kozi na ni mojawapo ya sababu zinazochangia ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana. Wanapaswa kufanya taaluma wanayotaka, ingawa kwa kushauriwa,” ahimiza Bi Purity Wanjiru ambaye ni daktari na mzazi.

Mtaalamu huyo anasema ufanisi wake katika taaluma anayofanya ulitokana na uungwaji mkono wa wazazi wake.

Bw Antony Mwangi anasema mapenzi yake yalikuwa kufanya kozi inayohusiana na masuala ya biashara, akiwa na lengo na maazimio ya kuwekeza kwenye biashara siku za usoni.

Kazi ya utingo, pia makanga ina pandashuka zake na kulingana na Antony wiki isingeisha bila kupelekwa seli kwa sababu ya ukiukaji wa makosa ya trafiki.

“Sekta ya uchukuzi, hasa matatu si rahisi. Nilipokata kauli kuiacha sikushinikizwa na yeyote,” adokeza.

Mnamo 2012, kwa mtaji wa Sh2,000 aliingilia uchuuzi wa nguo haswa za wanawake. Biashara hiyo ilinoga na kustawi. Ni kupitia mwanya huo ambapo Antony aliweza kuwekeza katika biashara ya uuzaji wa filamu na kanda za muziki.

Anasema gange hiyo ilishika kasi 2013 kiasi cha kumuwezesha kununua tuktuk mwaka uliofuata. Kwa kuwa teknolojia inaendelea kukua kila uchao, watu wanatoa nyimbo na filamu kwenye mitandao. Anaambia ‘Taifa Leo’ kwamba hakuwa na budi ila kufunga duka la shughuli hiyo.

Kwa usaidizi wa mapato ya tuktuk, 2016 aliweka duka ambalo ndilo afisi yake kufikia sasa. Duka hilo pia lina huduma za M-Pesa.

“Moyo sasa umetulia kwenye biashara kwa kuwa ndiyo ilikuwa matamanio yangu tangu nikiwa mdogo,” akasema wakati wa mahojiano.

Mfanyabiashara huyo anasema hakuna jambo muhimu kama matakwa ya mtoto, hususan taaluma anayopania kusomea, kuheshimiwa.

Anaongeza kueleza kwamba iwapo wazazi wake wangetilia maanani ndoto zake angewekeza kwenye biashara muda aliotumia kusomea umekanika ikiwa ni pamoja na aliokuwa makanga.

Antony Mwangi akiwa kwenye duka lake eneo la Mumbi, eneobunge la Ruiru katika Kaunti ya Kiambu. Picha/ Sammy Waweru

Kauli yake inapigwa jeki na Irene Maina, ambaye ni mama wa mtoto mmoja. Kulingana na Irene, bintiye mwenye umri wa miaka tisa ana kipaji cha sanaa, utengenezaji wa bidhaa za mapambo.

Mama huyo anapigia upatu mfumo mpya wa elimu ya uamilifu, maarufu kama CBC akieleza kwamba inasaidia kukuza talanta za watoto, tangia wakiwa wachanga.

“Msichana wangu anaelekea gredi ya nne 2020, kufikia sasa anajua kutengeneza bidhaa za mapambo kwa shanga na hata kufuma vikapu,” asema Binti Irene.

Anasema chini ya mtaala wa CBC, wanafunzi wanapaliliwa vipaji kwa mujibu wa uwezo wao. Ni kupitia mfumo huo ambapo watoto pia wanafunzwa mapishi pamoja na umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Bw Antony Mwangi anasema mwanambee wake – kifungua mimba – anaonekana kufurahia soka, kipaji anachosema anajaribu juu chini kukipalilia. “Wakati wa ziada anapenda kucheza kabumbu,” asema mfanyabiashara huyo.

Ili kupanua biashara yake, anapania kufungua duka la uuzaji wa bidhaa kwa kijumla. Amebuni nafasi kwa vijana wawili; msaidizi wake dukani na dereva wa tuktuk.