Makala

RIZIKI: Maisha yanahitaji mja awe mbunifu

October 17th, 2020 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

FRESHIER Mutheu, 41 alianza biashara yake ya kazi za sanaa katika mtaa wa Lanet, Nakuru wakati wa janga la COVID-19 kikiwa ni kipindi ambacho mapato kutokana na mauzo ya nguo yalipungua pakubwa.

“Nilianza biashara hii wakati huu wa janga la Covid-19,” anasema Methu.

Zuio la kuingia Nairobi pia lilimwathiri kwa njia hasi.

Hali hii ilimwacha Mutheu bila riziki na biashara yake ya uuzaji nguo ilikuwa ikipata hasara kubwa kutokana na athari za janga la Covid-19 na mwishowe akaifunga.

Jambo ambalo lilikuja akilini mwake ilikuwa talanta yake ya sanaa ya ubunifu.

“Wazo hili la ubunifu lilinifurahisha sana na mimi pamoja na mfanyakazi mahiri wa kunisaidia tulianza na kupamba vitabu. Nilikuwa na Sh3,000 kama mtaji na hela hizo zilitosha kuchapisha nakala 100,” anaeleza.

Mutheu, kama mwandishi na msomaji wa vitabu, alijua umuhimu wa kuwa na alamisho kadhaa. Ndivyo alianza biashara yake.

“Nilianza kutengeneza pia kadi kutoka kwa mauzo ya vitu hivi viwili, niliweka alama kwa vikombe vichache na kutoka hapo nilifanya fremu za picha ambazo ni maarufu sana kwenye soko na nilianza kufanikiwa,” Mutheu anasema.

Anaongeza: “Ninapenda rangi. Ninapenda kuwa na mada na picha tofauti na vilevile ujumbe wa kutia moyo na ninachapisha kwenye fremu, kadi spesheli, vikombe na mashati. Hivi ndivyo Freshier Design Collections ilivyoanza. Na biashara yangu ni mkusanyiko wa miundo yangu ambayo sasa inafanya vizuri katika soko.”

 

Frashier Mutheu anaonyesha baadhi ya bidhaa zake katika mtaa wa Lanet, Nakuru Julai 29, 2020. Picha/ Margaret Maina

Mutheu hutumia majukwaa ya kijamii kuzungumza, kuhamasisha na kuwapa ushauri watu juu ya stadi za maisha, maswala ya uongozi, uzazi na ujasiriamali.

“Mtu lazima aondoe mawazo ya kuwa maskini na badala yake awe na mtazamo tofauti maishani,” anasema.

Amechapisha kitabu ‘Unstuck’ kinachoshauri watu kutazama maisha kutoka pembe tofauti na kutumia talanta zao na kufahamu “unachohitajika kufanya ili kuukabili na kuushinda umaskini”.