Makala

RIZIKI NA MAARIFA: Amekuwa na wengi mifugo, lakini aungama sungura ndio 'kitu' bora kwake

October 3rd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA na CORNELIUS MUTISYA

SAFARI yetu ya kikazi ilianza saa mbili asubuhi.

Tuliabiri bodaboda kutoka mjini Machakos na tukafika katika kitongoji duni cha Kitulu, kata ya Kaewa, kaunti ya Machakos, kukutana na mfugaji sungura wa kipekee hapa Carol Mutheu kulingana na miadi aliyotupa majuma mawili yaliyopita.

Amekuwa fahari kuu na kivutio kwa wakazi wa hapa kutokana na kazi hii ambayo humwingizia maelfu ya pesa kila mwaka.

Bi Mutheu adokeza kwamba, aliamua kujitosa mzimamzima katika mradi wa ufugaji sungura kama mradi wa ziada.

Hii ni kwa sababu awali akijishughukisha na kilimo cha viazi vikuu (nduma), mboga na matunda, ufugaji wa mbuzi wa kienyeji, ng’ombe, nguruwe na kuku akisaidiana na mumewe Bw Kimeu Mutune.

Kimeu Mutune aliye dereva msifika wa magari ya uchukuzi janibu za Ukambani. Miradi hiyo yote ilimfanya awe kielelezo chema kwa jamii.

Hata hivyo, Mama Mutheu asema kwamba, imempambazukia kuwa ufugaji wa sungura ni nafuu na hauna hasara kwa mkulima ilhali una mapato mazuri ikiwa mkulima atafuata kikaamilifu maagizo kutoka kwa wataalamu wa ufugaji.

“Ufugaji wa sungura una faida mno siku hizi. Hata hivyo, sio wakulima wengi wametambua tija ya kuanzisha kazi hii ashirafu,” anasema.

Bi Mutheu ambaye ni mama wa watoto wawili asema kwamba, nyama ya sungura ndiyo iliyo bora zaidi kwa sababu ina madini mengi ya protein kuliko nyama zozote zile.

“Nyama ya sungura ina protein nyingi na waka haina mafuta mengi kama ya ng’ombe na nguruwe,” aarifu mkulima huyu msifika.

Asema kwamba, aliamua kuingilia ufugaji wa sungura miaka minne iliyopita na hajuti asilani. Hii ni kwa sababu biashara ya kuuza sungura imenoga mno masokoni na huwa inamletea faida nzuri.

“Huwa natia kibindoni takribani Sh100,000 kwa mwaka kupitia biashara ya kuuza sungura kwa ajili ya nyama. Wateja wangu wakubwa ni wamiliki wa hoteli na maduka ya jumla mjini Machakos’’ asema Bi Mutheu.

Anafichua kuwa, sungura hukua haraka sana kuliko wanyama wake wengine. Sababu ni kwamba sungura ukomaa akifikisha kati ya miezi 4-5 na kuwa tayari kupelekwa sokoni.

Si hayo tu, mwanamke huyu gangari anaongeza kuwa, sungura huzaa baada ya muda wa miezi miwili na hivyo idadi yao huongezeka haraka

Faida nyingine ya ufugaji wa sungura ni unahitaji kuanzishwa kwa mtaji wa kiasi kidogo cha pesa.

“Ingawa niliwekeza mtaji wa Sh3,000 pekee katika mradi huu miaka minne iliyopita, sasa ninachuma takriban Sh100,000 kila mwaka kabla ya kuondoa gharama,” Bi Mutheu anaeleza.

Aidha, Mutheu asema kwamba, sungura hulishwa kwa majani ya mimea tofauti, nyasi na hata mabaki ya jikoni na hivyo mkulima huwa hapati huwa habebi gharama kubwa ya lishe.

Mkulima huyo hufuga sungura aina mbalimbali kama vile, “California White”, “Flemish Giant” na “New Zealand White”.

Sungura huhitaji kufugwa katika kibanda safi na chenye hewa mwanana na pia kilichojengwa kwa mbao na nyaya imara na thabiti ili kuepuka wanyama waharibigu kama mbwa mwitu, paka shume na hata wezi.

Faida nyingine ya sungura, kulingana na Mutheu, ni kwamba mkojo wa sungura umethibitishwa na wataalamu wa kiafya kuwa na chembechembe za kutibu magonjwa sugu kama mkimbio wa damu.

Aidha, ngozi yake inaweza kutumiwa kuwamba ngoma, kutengeneza mishipi na hata kuunda nakshi za kurembesha nyumba.

Bi Mutheu anasema sifa zake za ufugaji wa sungura sasa zimevuma maeneo kadhaa katika kaunti ya Machakos kiasi kwamba maafisa wa ufugaji wa mifugo nyanjani hutembelea mara kwa mara.