Makala

RIZIKI NA MAARIFA: Utingo mwanamke aliyejipata katika ajira hiyo kwa njia asiyotarajia

September 12th, 2019 2 min read

Na STEPHEN ODANGA

BI Mary Taka Ochum, 47, mama wa watoto watatu amekuwa akifanya kazi ya utingo tangu mwaka wa 2007.

Anafahamika zaidi kama ‘Nairobi Bus’ kwa sababu anafanya kazi kwa mabasi ya kuelekea Nairobi.

Anasimulia kwamba alianza kazi ya utingo bila kutarajia, na hii ni wakati alikuwa akimpeleka mwanawe aliyeumia hospitalini kwa matibabu kila siku ndipo akajifunza kazi hii.

Anasema wakati alikosa nauli ya kuenda hospitalini, dereva wa gari alilokuwa akisafiria kila siku alimwambia ajaribu kurai wasafiri waingie kwenye gari ndipo aweze kubebwa hadi hospitalini bila kulipishwa nauli.

Alifanya jinsi alivyoambiwa na ikawa hivyo kila siku, aliweza kuingiza abiria wengi kwenye gari jambo lililosababisha dereva huyo kumwajiri kama utingo kwa gari hilo aina ya matatu.

Mary anazidi kufichua kwamba hapo mwanzoni alikuwa fundi wa nguo mjini Port Victoria, kaunti hii ya Busia, lakini kwasababu ya safari za kila siku hakuweza kuketi kwa cherehani kushona. Kuweka msumari wa moto kwenye kidonda, mumewe pia alitoroka baada ya mtoto kuumia vibaya.

Anaeleza kuwa alizidi kufanya kazi ya utingo kila siku wakati akimpeleka mtoto kwa matibabu hospitalini hadi akazoea. Anaongeza kusema alipata pesa nyingi za haraka kwa kazi hii ya utingo jambo lililomtia motisha zaidi.

Mtoto alipopata nafuu, alimpeleka kwa mamake mzazi amsaidie kumtunza huku yeye akiendelea na kazi ya kutafuta pesa.

Kina mama wenzake walimkejeli na kumuona kama amechanganyikiwa na maisha kwa kufanya kazi ya utingo lakini hakuwasikiza.

Aliongeza bidii kwa kazi hii ambayo anasema hunoga zaidi msimu wa Disemba na Januari huku akiisifu kuwa kazi ambayo huwezi kulala njaa hata siku moja.

Ushonaji

Mwaka wa 2008, akiwa bado anaendelea na kazi ya utingo aliweza pia kuajiriwa kazi ya kushona sare za shule katika Shule ya Upili ya Wasichana ya St Cecilia Nangina, Kaunti ya Busia. Aliajiriwa kushona sare za shule kwa sababu alikuwa fundi mahiri anayesifika eneo hilo.

Anasema alikuwa akienda kufanya kazi ya kushona nguo wakati wa ziada, akiwa hayuko kwa kazi ya utingo.

Kazi yake ya utingo ilinoga sana wakati akiwa anashona sare za shule.Wakati shule zafungwa alikuwa akikusanya nauli kwa wanafunzi wa shule hiyo na kuleta gari la kuwabeba kwa pamoja hadi makwao na kujipatia pesa nyingi.

Mama Mary amedhihirisha methali isemayo “Hamadi kibindoni, silaha iliyo mkononi”. Methali hii inaonya kuwa tuwe tayari maishani kwasababu lolote laweza kufanyika.

Bidii yake imemwezesha kununua ploti na kujenga nyumba kubwa ya mawe kando na kumlipia mwanawe mkubwa karo ya shule kwa kidato cha pili sasa.

Anahimiza kina mama wengine ambao wameachiwa majukumu ya kulea watoto wenyewe kuwa wapanue mbawa zao. Wakiwa na mapato madogo wasife moyo wajibidiishe kwa kila kazi wanazoweza kufanya ili kukimu maisha.

Mama Mary anafanya kazi kwa kampuni ya magari ya uchukuzi ya Nairobi Bus, kituo cha magari cha Nangina, eneobunge la Funyula, kaunti ya Busia.