Makala

RIZIKI: Uchoraji wamvunia donge na kumpa tonge

May 8th, 2020 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MCHORAJI Robert Chumbi, 28, huvutia wapitanjia na picha anazochora.

“Kama msanii, mojawapo ya njia bora za kuonyesha talanta ni kwenye kipande cha turubai. Kutoka kwa uchoraji wa rangi za mafuta hadi picha za turubai, kuna kitu tu juu ya nyenzo hii ambacho kinampa mchoraji fahari,” anasema Robert.

Mzaliwa wa Nanyuki, Robert anasema kwamba baada ya kukamilisha elimu ya shule ya sekondari alianza kuuza viatu jijini Nairobi kujipatia riziki lakini baadaye akahamia Mombasa kuwa mekanika wa pikipiki na baadaye kuwa wakala wa nyumba.

Robert Chumbi akichora. Picha/ Margaret Maina

Lakini hamu yake ya kufanya kazi za sanaa haikumruhusu kuzingatia mambo mengine na mnamo 2012 alirudi Nairobi na kupitia rafiki yake, alijifunza kutengeneza sanamu za wanyama.

“Nilianza kuchora vitu tofauti kwa kutumia penseli tangu utotoni. Na ingawa nilijifunza kuchonga sanamu za wanyama, mapato hayakuwa mazuri kwa hapakuwepo soko nzuri na ilichukua muda mrefu sanamu kukauka,” anasema.

Robert aliamua kuhamia kabisa kwenye turubai; uamuzi ambao hajutii.

“Nilikuwa na pahali pa kuonyesha sanaa yangu Kinoo lakini nilikuwa nikisafiri kwenda Nakuru kuuza vipande vyangu na faida ilikuwa ya kuvutia .”

Robert, pamoja na rafiki yake kwa jina Samwel Kinuthia walihamia Nakuru Januari 2019.

Michoro mbalimbali ambayo ni kazi yake Robert Chumbi. Picha/ Margaret Maina

Robert ambaye sasa ana wafanyakazi watatu anasema kwamba huuza kazi zake za michoro kuanzia Sh1,000 hadi Sh15,000 na hupata faida ya angalau Sh60,000 kwa mwezi ambao biashara huwa mzuri.

Licha ya ufanisi huo, anakumbana na changamoto tofauti.

“Tunafanya kazi nje na wakati kunanyesha lazima tufunge kazi; hali inayofanya michoro yetu kuchukua muda mrefu kukauka,’’ anasema.

Wateja wake ni wanasiasa na mwananchi wa kawaida vilevile. Wingi huu wa wateja umemfanya Robert kuwa mbunifu zaidi.

Huwa pia anawalenga watalii wawapo njiani na barabarani kuelekea Ziwa Bogoria.

Matarajio yake ni kumiliki studio katika siku zijazo na kupanua soko lake kwa miji tofauti.

“Katika tasnia hii, ni muhimu sana kwa wasanii kupata msaada na ushauri kutoka kwa wasanii wakubwa kwani ni rahisi mtu kukata tamaa,” anasema.