Makala

RIZIKI: Utingo aliyejipanga akawekeza kwenye biashara ya tuktuk

February 6th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

BAADA ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, mnamo 2004, Duncan Kinuthia alitafuta mbinu za kujitafutia riziki.

Akiwa mzaliwa wa Murang’a na ambako pia alisomea, Kinuthia alikita kambi jijini Nairobi kusukuma gurudumu la maisha.

“Nilikuwa na jamaa na marafiki katika mtaa wa Kariobangi na ambao walinipokea,” anaeleza Kinuthia.

Nairobi husemekana ni shamba la mawe, na mfuko wa mwanamume ndio shamba lake. Kinuthia anasema hakuwa na budi ila kufanya vibarua vya hapa na pale, angaa aweze kupata tonge la mlo.

“Nilipewa makazi kwa muda, chakula, mavazi na mahitaji mengine sharti ningejishughulikia,” aelezea.

Kulingana na barobaro huyo alijiunga na kundi moja la vijana lililokuwa likiosha magari eneo la Kariobangi.

Kwenye simulizi yake, Kinuthia anasema gange ilikuwa yenye mapato.

Kwa siku, angefanikiwa kupata zaidi ya Sh1,500.

“Baada ya kuondoa mahitaji yote, ikiwamo kodi ya nyumba na chakula nilikuwa naweka akiba isiyopungua Sh500 kila siku,” afichua.

Miaka mitatu baadaye, Kinuthia alijiunga na sekta ya matatu kama utingo, maarufu kama kondakta au makanga.

“Kwa muda wa miaka hiyo, nilikuwa nimetangamana na wamiliki na wahudumu wengi wa matatu. Pia niliweza kupitia mafunzo ya udereva,” anaeleza.

Huo ulikuwa mwishoni mwa mwaka wa 2007.

Kinuthia anaiambia Akilimali kwamba alihudumu kama utingo kwa muda wa miaka saba mfululizo.

Bw Duncan Kinuthia mmiliki na mhudumu wa tuktuk eneo la Githurai. Wakati mmoja Kinuthia alikuwa mwosha magari na utingo. Aliweka akiba na hatimaye akafanikiwa kununua tuktuk. Picha/ Sammy Waweru

Kijana huyo aliendeleza mazoea ya kuweka akiba, hata ingawa kuna baadhi ya siku au hata wiki mapato yangekuwa haba.

Uwekaji akiba ni mojapo ya mbinu inayotiliwa mkazo, hasa ikiwa mmoja ana chanzo cha mapato. Ili kupiga jeki mapato yako, unahitaji kuwa na njia mbadala kama vile kuwekeza katika biashara, ununuzi wa ploti na ujenzi.

“Mara kwa mara huhimiza vijana kukumbatia wazo la kuweka akiba licha ya kiwango cha mapato yao. Wanaweza kujiunga katika makundi, mashirika ya kifedha kama benki au vyama vya ushirika, ndivyo Sacco,” ashauri Dennis Muchiri, mtaalamu wa masuala ya fedha na uchumi.

Mdau huyo hata hivyo anasifia umuhimu wa kujiunga na Sacco, akihoji huduma zake ni nafuu ikiwamo utozaji wa riba ya chini katika mikopo. “Baada ya kuweka akiba kwa muda, unaweza kuomba mkopo uutumie kujiimarisha,” Muchiri asema.

Duncan Kinuthia anasema alikuwa katika kundi la vijana ambao walikuwa wakiweka akiba kwenye chama kimoja cha ushirika Nairobi. Kufikia mwaka 2014, kijana huyo anasema alikuwa ameweka kibindoni kima cha pesa kilichomuwezesha kupata mkopo.

“Niliuchukua kupitia dhamana ya akiba yangu na vijana kadha walionisimamia, nikanunua kijigari kidogo aina ya tuktuk,” anadokeza. Licha ya hatua hiyo, hakugura kazi ya ukondakta.

Hata hivyo, anasema huduma ya uchukuzi hususan matatu ni sekta yenye changamoto chungu nzima, ikizingatiwa kuwa maafisa wa trafiki huyatafutia magari makosa madogo madogo.

“Si mara moja, mbili au tatu nimelala seli nikiwa makanga. Kimsingi, ni sekta yenye pandashuka tele. Kumbuka, mmiliki lazima apate mshahara nami na dereva tujilipe, pamoja na wanaoshawishi wasafiri kuingia,” afafanua.

Mnamo 2018, baada ya kukamilisha kulipa mkopo, Kinuthia anasema alipungia kwaheri kazi ya utingo, akaingilia kikamilifu huduma za tuktuk. Huendeshea shughuli hiyo eneo la Githurai na Mwihoko.

Wakati wa mahojiano alisema kijigari hicho hakina gharama ya juu vile.

Kwa mfano, utumizi wa mafuta alisema kwa siku hugharimu takribani Sh700, kiasi ambacho kinaweza kuingiza zaidi ya Sh2,500.

Isitoshe, vipuri vya tuktuk vinauzwa kwa bei nafuu na ambapo pia gharama ya kutunza kijigari hicho ni ya chini. Tuktuk imeundwa kubeba abiria watatu, japo hukarabatiwa kusafirisha jumla ya watano.

Nauli yake ni nafuu pia, kwani kati ya Mwihoko na Githurai msafiri hulipa kati ya Sh30 – 50.

Masafa mafupi, wahudumu hutoza kadri ya Sh20.

Kinuthia anasema anapania kuongeza tuktuk nyingine, katika mpangilio wa ruwaza yake ya muda wa miaka mitano ijayo.