Riziki: Wamlilia Ruto awatoe kwa ukahaba

Riziki: Wamlilia Ruto awatoe kwa ukahaba

Na WACHIRA MWANGI

KIKUNDI cha wanawake wanaofanya kazi ya ukahaba katika Kaunti ya Mombasa, wamemwomba Naibu Rais William Ruto awasaidie kuanzisha biashara tofuati itakayowainua kimaisha.

Wito wao umetokana na ahadi ambayo Dkt Ruto alitolea makahaba alipokuwa katika ziara Kaunti ya Makueni mnamo Oktoba, ambapo aliwaahidi Sh1 milioni za kuanzisha biashara.

Naibu Rais alikuwa ametoa ahadi hiyo kufuatia ombi la wanawake ambao walimwambia wamejitolea kufanya biashara mbadala za kujitafutia riziki ili waachane na ukahaba.

Baadhi ya makahaba katika Kaunti ya Mombasa waliamua kujaribu bahati yao ili wao pia wanufaike na ukarimu huo wa Naibu Rais, lakini sasa wanalalamika imekuwa vigumu kumfikia.

Wanawake hao 33 ambao hufanya shughuli hizo katika mtaa wa kifahari wa Nyali wana kikundi chao cha kijamii kilichosajiliwa, ambacho walikuwa wamenuia kutumia kutafuta nafasi za uwekezaji wa biashara ndogondogo.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao, Bi Consolata Kendi, walisema wamejaribu kila njia kupata kikao na Dkt Ruto ili wawasilishe pendekezo lao la kibiashara, lakini wapi!

“Tunaomba tu kukutana naye ili tumweleze kuhusu pendekezo letu la biashara mbadala, ndipo atusaidie jinsi alivyofanyia wenzetu Makueni,” akasema Bi Kendi.

Pendekezo hilo lililoandikwa kwa umakinifu wa kibiashara unaeleza mpango wa kuwekeza katika kazi za urembeshaji na utiaji nakshi katika mtaa wa Nyali.

Bi Kendi alisema biashara hiyo ikifana haitakuwa kwa manufaa kwa wanachama pekee bali pia itatoa nafasi za ajira kwa wanajamii wengine.

Alieleza kuwa changamoto wanazopitia katika ukahaba ziliwafanya waanze kuwazia upya kuhusu maisha yao.

“Hii biashara itatuondoa katika umasikini, kukamatwa kiholela na kuhangaishwa na polisi na pia hatari ya kuambukizwa maradhi kama vile Ukimwi,” akasema.

Kulingana naye, mpango wao unaenda sambamba na mfumo wa kiuchumi wa ‘bottom-up’ ambao hushabikiwa na Dkt Ruto na wafuasi wake kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Wakati Naibu Rais alikuwa Makueni mnamo Oktoba, alishauri wanawake wanaofanya ukahaba waungane katika makundi na wasajili vyama vya ushirika (Sacco), ambapo angewapa Sh1 milioni za kuanzisha biashara ili wafanye kazi halali.

Alitoa ahadi hiyo baada ya kupokea ombi la mwanamke aliyedai kuwa ni kahaba, na alitaka usaidizi pamoja na wenzake kuanzisha biashara rasmi kwani wanakumbana na changamoto nyingi kando na unyanyapaa wa kufanya ukahaba.

“Inachukua mtu jasiri na shujaa kusimama mbele ya Naibu Rais kusema ‘mimi nafanya biashara fulani’. Inamaanisha kweli hawa kinamama wanataka usaidizi.. Mimi nawaambia kuwa nitawasidia mfanye biashara nyingine,” Dkt Ruto alisema wakati huo.

Baadhi ya wakosoaji wake kisiasa walimkashifu kwa hatua hiyo, wakidai ni kama sawa na kuhalalisha shughuli iliyoharamishwa kisheria.

Hata hivyo, wandani wake walisema ni ukarimu wa Naibu Rais kujitolea kusaidia wananchi wa ngazi za chini bila ubaguzi.

“Kazi ya kiongozi ni kutoa suluhu. Hata Biblia inasema mtoto akililia mkate hufai kumpa jiwe,” alisema Mbunge wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua.

You can share this post!

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Kukuza na kuendeleza Kiswahili...

Serikali iharakishe miradi ya Italia – Kingi

T L