Michezo

Rodgers azima ndoto ya Sheffield

July 21st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MATUMAINI ya Sheffield United ya kushiriki soka ya bara Ulaya msimu ujao yalizamishwa na Everton waliowapokeza kichapo cha 1-0 mnamo Julai 20, 2020 uwanjani Bramall Lane.

Katika mechi nyingine, Wolves walidumisha maazimio ya kunogesha kipute cha Europa League muhula ujao kwa kuwalaza Crystal Palace 2-0 uwanjani Molineux. Ufanisi huo wa vijana wa kocha Nuno Espirito uliwakweza hadi nafasi ya sita jedwalini kwa alama 59, moja mbele ya Tottenham Hotspur.

Richarlson alifungia Everton bao la pekee na la ushindi kwenye mchuano huo katika kipindi cha pili baada ya kushirikiana vilivyo na kiungo Gylfi Sigurdsson.

Goli hilo lilichangia msisimko kiasi katika mechi hiyo iliyoshuhudia kila kikosi kikibana sana safu yake ya ulinzi huku jaribio la pekee la Everton langoni katika kipindi cha kwanza likitokana na kombora la Dominic Calvert-Lewin kunako dakika ya 24.

Ushindi wa Everton katika mechi hiyo ulizamisha kabisa matumaini finyu ya Sheffield United ya kukamilisha kampeni za muhula huu ndani ya mduara wa sita-bora na hivyo kufuzu kwa kivumbi cha Europa League msimu ujao.

Kufikia sasa, Sheffield United wanashikilia nafasi ya nane kwa alama 54 sawa na Burnley ambao watafunga kampeni za EPL msimu huu dhidi ya Brighton uwanjani Turf Moor. Sheffield United watakamilisha kivumbi cha muhula huu dhidi ya Southampton ugani St Mary’s.

Everton waliopaa hadi nafasi ya 11 kwa alama 49 sawa na Southampton, wamepangiwa kupepetana na Bournemouth uwanjani Goodison Park.

Ushindi kwa Wolves dhidi ya Chelsea katika mchuano wao wa mwisho mnamo Julai 26 ugani Stamford Bridge utawapa tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki Europa League. Mabao ya Wolves yalifumwa wavuni kupitia kwa Daniel Podence na Jonny Otto.

Kwingineko, Brighton walijihakikishia kuwa watakwepa kushuka ngazi mwishoni mwa msimu huu katika EPL baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya Newcastle United uwanjani Amex.

Brighton walishuka uwanjani kwa ajili ya mechi hiyo wakihitaji alama moja pekee ili kuweka hai matumaini ya kusalia ligini msimu ujao.

Sare hiyo iliwapaisha Brighton hadi nafasi ya 15 jedwalini kwa alama 38, saba zaidi kuliko Bournemouth ambao wananing’inia padogo zaidi mkiani sawa na Norwich City ambao tayari wameteremshwa ngazi. Newcastle wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama 44, tisa nyuma ya Arsenal ambao watamenyana leo Aston Villa ugani Villa Park.

Brighton kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Burnley katika siku ya mwisho ya msimu huu huku Newcastle wakiwaalika mabingwa Liverpool.

MATOKEO YA EPL (Julai 20, 2020):

Brighton 0-0 Newcastle United

Sheffield United 0-1 Everton

Wolves 2-0 Crystal Palace